Pasta asumilia kumezwa mzima kisha kutemwa na simba baada ya dakika 45 (video)

Alisisitiza kwamba yeye ni miongoni mwa watu wachache duniani kote ambao wanafahamu tarehe na muda kamili ya urejeo ya Yesu kristo duniani.

Muhtasari

• "Sijui vile ilitokea lakini tulianza kusikia sauti za simba na tuliogopa sana. Waliniambia mimi ndio mchungaji niwaweke kwa maombi.”

Pasta William Ssozi
Pasta William Ssozi
Image: Screengrab

Mchungaji mmoja kutoka taifa jirani la Uganda ambaye anajiita Nabii wa Mungu William Ssozi amewashangaza wengi baada ya kufanya mahojiano na runinga ya UBC na kusimulia kile ambacho anasema ni kumezwa na kisha kutemwa na simba.

Nabii huyo anaonekana akifafanua kuwa alimezwa na Simba akiwa katika siku zake za mwanzo za Utumishi katika sehemu moja ya Afrika Kusini na anaendelea kusema kuwa ni kwenye tumbo la simba ambapo alijifunza kutabiri.

“Nchini Afrika Kusini ndiko nilishuhudia kitu cha kunibadilisha kabisa kimaisha. Nilimezwa na simba. Tulikuwa tumeenda kutembea mbugani, na gari letu liliisha mafuta katikati ya mbuga. Sijui vile ilitokea lakini tulianza kusikia sauti za simba na tuliogopa sana. Waliniambia mimi ndio mchungaji niwaweke kwa maombi.”

“Simba akaja na kati ya marafiki zangu wote, simba alinichagua mimi tu na kunimeza. Na tumboni mwa simba ndipo Mungu alinijia na kunizungumzia, na kuniambia jinsi nitakavyoanza kutoa unabii kwa undani Zaidi,” aliongeza.

"Nilikuwa na shule yangu ya Unabii katika tumbo la simba."

Kulingana na nabii huyo, alimezwa na kisha simba kumtema akiwa hai na mzima lakini alibaki na kovu moja tu dogo ambalo lilitokana na jino la Simba kuteleza katika mkono wake wa kushoto.

Kando na kisa hicho ambacho wengi wanaona kama ‘stori za jaba’, mchungaji huyo pia alimshangaza mtangazaji akisema kwamba aliwahi kwenda mbinguni na kukutana na Mungu pasi na kufa.

“Nimewahi kwenda mbungini, sikufa, nilikuwa hai. Nimekuwa mbinguni si mara moja bali mara kadhaa tu, na nilienda kimwili na Mungu akanitawaza kama nabii.  Wakati nikienda mbinguni, sikujua kwa nini nilienda kule hadi nilipokutana na Mungu na kunieleza kusudio lake,” alieleza.

Alisisitiza kwamba yeye ni miongoni mwa watu wachache duniani kote ambao wanafahamu tarehe na muda kamili ya urejeo ya Yesu kristo duniani.