Wanangu hawajaoa na wanatafuta wapenzi - Rais mstaafu wa Ghana John Mahama afichua

Rais huyo alitambulisha wavulana wake wawili na binti mmoja na kuweka wazi kwamba wavulana wote wako single na wanatafuta warembo wazuri kufunga ndoa nao.

Muhtasari

• Rais huyo wa zamani alitembelea hospitali moja na familia yake kama njia moja ya kusherehekea kufikisha miaka 65.

Rais wa zamani John Dramani Mahama na familia yake
Rais wa zamani John Dramani Mahama na familia yake
Image: Facebook

Rais wa zamani wa Jamhuri ya Ghana, John Dramani Mahama, amewachekesha watu baada ya kufichua kwamba vijana wake wawili watanashati bado wako single na wako sokoni wanatafuta warembo wa kuwaoa.

Mahama, baba wa wavulana wawili, Sharaf na Shahid Mahama alisema wawili hao hawajaoa na wanasaka wasichana.

Ili kuadhimisha miaka 65 ya kuzaliwa kwake, Rais wa zamani wa Ghana, John Dramani Mahama aliamua kuchangia baadhi ya pesa na vitu kwa hospitali ya Wilaya ya Shai Osudoku pamoja na mkewe na watoto.

Alitumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa hospitali hiyo kwa kulitunza jengo ambalo serikali yake ilijenga wakati akiwa madarakani.

Aidha, Bw. Mahama alipongeza hatua iliyofikiwa na hospitali hiyo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita katika kuweka idadi ya vifo vya wajawazito kuwa chini.

Alitangulia kuwatambulisha watoto hao kwa wauguzi na wafanyakazi waliokuwepo na kuwafunulia kwamba wanawe wawili watanashati hawajaoa na wanatafuta warembo wazuri wa kuwaoa, jambo ambalo lilipokelewa na watu kwa shangwe na vifijo.

“Sharaf Mahama ako hapa, na pia Shahid Mahama yuko hapa. Na pia binti yangu Farida yuko hapa ila mtoto wa mwisho kwa familia yangu hayuko hapa. Ningependa kuwashukuru nyote lakini pia niwaambie kwamba wavulana wangu wako single,” Mahama alisema watu wakishangilia.