Nesi wa Kiafrika afutwa kazi na kufukuzwa UK kisa kufanya maombi kwa mgonjwa mahututi

Daktari mwenzake alieleza kwamba nchini UIngereza, ni kinyume cha sheria mhudumu wa afya kuleta udini kazini kuwaombea wagonjwa, na kama inabidi, anafaa kuwahusisha viongozi wa kidini tu!

Muhtasari

• Alieleza kuwa inachukuliwa kuwa ni kinyume cha maadili kwa wahudumu wa afya au wauguzi kuleta dini katika kazi zao.

• Aliongeza kuwa hata mgonjwa akiomba muuguzi awaombee, muuguzi huyo anapaswa kumwalika padre au kasisi kufanya maombi hayo badala ya kufanya wao wenyewe.

Nesi
Nesi
Image: BBC NEWS

Muuguzi mmoja raia wa Nigeria ameripotiwa kufutwa kazi na kufukuzwa nchini Uingereza baada ya kuripotiwa kufumaniwa akimuombea mgonjwa mahututi anayekaribia kufa.

Kulingana na mtumizi wa mtandao wa X, ambaye anajitambulisha kama daktari kutoka taifa hilo la Afrika Magharibi kwa jina Dkt. Olufunmilayo, ambaye alishiriki tukio hilo kwenye mitandao ya kijamii, inadaiwa muuguzi huyo alipatikana na hatia ya kumwombea mgonjwa, jambo ambalo linachukuliwa kuwa halikubaliki katika mfumo wa afya wa Uingereza.

Alieleza kuwa inachukuliwa kuwa ni kinyume cha maadili kwa wahudumu wa afya au wauguzi kuleta dini katika kazi zao.

Aliongeza kuwa hata mgonjwa akiomba muuguzi awaombee, muuguzi huyo anapaswa kumwalika padre au kasisi kufanya maombi hayo badala ya kufanya wao wenyewe.

Alishiriki hadithi hiyo mtandaoni kuwaonya wahudumu wa afya wa Kiafrika wanaohamia Uingereza dhidi ya kuwaombea wagonjwa ili kuepuka kukabiliwa na hali kama hiyo.

Soma tweet yake kamili hapa chini,

"Nimetoka tu kusoma hadithi ya kusikitisha ya Mnigeria aliyekuja uingereza aliyeajiriwa na wakala kufanya kazi ya kuwatunza wazee. Alipewa jukumu la kumtunza mgonjwa mzee ambaye alikuwa karibu kufa na aliripotiwa "kuombea mteja kupata nafuu". Ndiyo. Alifukuzwa kazi na kufukuzwa Uingereza.”

“Kwa wale wanaoonyesha kushtushwa na suala la kufukuzwa, wacha nieleze zaidi. Kama mhudumu wa afya nchini Uingereza, ni kinyume cha maadili kuhusisha dini au kulazimisha maoni yako ya kidini kwa wagonjwa/wateja.”

“Inachukuliwa kama matumizi mabaya ya uaminifu na matumizi mabaya ya nafasi yako. Unatarajiwa kufanya kazi yako tu na kuzingatia kazi yako. Hata kama mgonjwa/mteja angeleta mazungumzo ya kidini, unapaswa kuwaelekeza waongee na mchungaji, kasisi, imaam, kasisi au mtu yeyote wa kidini,” daktari huyo anayefanya kazi Uingereza alifafanua.

“Kama mfanyakazi wa afya; Hupaswi kujihusisha na shughuli za kidini na mgonjwa/mteja.  Ukiripotiwa kwa mamlaka husika, unaweza kupoteza kazi yako. Mara nyingi, hii inamaanisha pia kuwa umepoteza ufadhili wako na visa ya kusalia nchini. Kumbuka visa yako ya kukaa nchini kama mfanyakazi inafungamana na ajira yako. Ukipoteza ajira yako- utapoteza ukaaji wako nchini,” aliongeza.