Charlene Ruto miongoni mwa wanawake 100 wenye ushawishi mkubwa barani Afrika 2023

Charlene Ruto alijinafasi kwenye orodha hiyo ya ushawishi Afrika shukrani kwa wakfu wake wa Smachs, wakfu ambao umejikita Zaidi katika vita dhidi ya njaa ya tabianchi.

Muhtasari

• Smachs Foundation inalenga kuwaongoza vijana kuwa katika mstari wa mbele kushiriki vita dhidi ya njaa na mabadiliko ya tabianchi nchini Kenya.

Charlene Ruto
Charlene Ruto
Image: Facebook

Binti wa kwanza wa taifa, Charlene Ruto ni miongoni mwa wanawake 100 wenye ushawishi mkubwa Zaidi katika bara la Afrika katika mwaka wa 2023, haya ni kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa kwenye gazeti la Nation.afrika.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, bintiye rais Ruto ni miongoni mwa wanawake 9 tu kutoka nchini Kenya waliofanikiwa kujinafasi kwenye orodha hiyo ya wanawake 100 katika bara zima la Afrika.

Ripoti hiyo inasema kwamba Charlene Ruto alijinafasi kwenye orodha hiyo ya ushawishi Afrika shukrani kwa wakfu wake wa Smachs, wakfu ambao umejikita Zaidi katika masuala ya vijana na ambao haulengi kutengeneza faida kutoka kwa shughuli zake.

Smachs Foundation inalenga kuwaongoza vijana kuwa katika mstari wa mbele kushiriki vita dhidi ya njaa na mabadiliko ya tabianchi nchini Kenya.

Wanawake wengine Wakenya katika orodha hiyo ni pamoja na waziri wa mazingira Soipan Tuya, rubani wa kike wa shirika la ndege la Kenya, Irene Koki Mutungi, naibu katibu wa UN Global Compact, Sanda Ojiambo.

Wengine pia ni pamoja na jaji mkuu Martha Koome, Elizabeth Wathuti ambaye ni mwanaharakati wa kimazingira, Alice Wairimu Nderitu ambaye ni mshauri dhidi ya mauaji ya kimbari katika shirika la UN, Caroline Wanga ambaye ni CEO wa kampuni ya Essence Ventures na Racey Muchilwa - Mkuu wa Novartis Kusini mwa Jangwa la Sahara.