Nabii wa Kenya mwenye utata, Victor Kanyari mnamo Jumapili alisimulia kwa hisia kuhusu kifo cha uchungu kilichompata dadake mwenye umri wa miaka 26, Starlet Wahu.
Mwili wa Wahu, ambaye ni dada wa pekee wa nabii huyo, ulipatikana siku ya Alhamisi asubuhi baada ya kudaiwa kuuawa na mwanamume aliyetambulishwa kama John Matara ambaye alikuwa ameandamana naye katika chumba cha kukodi cha AirBnB mtaani South B, jijini Nairobi.
Wakati akisimulia kuhusu mauaji hayo, Kanyari alisisitiza kwamba dadake alijuana na muuaji wake kupitia mitandao ya kijamii na wawili hao wakakutana kujiburudisha.
“Ni kweli dada yangu alipata mwanaume na yule mwanaume akamchumbia mitandaoni. Na wakati alimdate katika mitandao, wakapendania huko kwa Facebook. Wakati walipendana yule mwanaume akamwalika akamwambia kuja tukule na tukunywe. Mwanaume akamwambia yeye ni tajiri sana, na wasichana wa siku hizi wanapenda matajiri,” Prophet Kanyari alisimulia.
Mtumishi huyo wa Mungu mwenye utata mwingi alibainisha kuwa dadake alikuwa mwanasosholaiti na alikuwa na wafuasi wengi sana kwenye mitandao ya kijamii.
“Sasa yule mwanaume akamuita. Wakaenda kwa klabu fulani wakakula nyama, wakakunywa pombe. Walipomaliza kula nyama na kunywa pombe, yule mwanaume akamwambia basi ningetaka tuwe na urafiki.
Wakakubaliana. Na wakakodisha nyumba ya kwenda kulala. Wakati wa kulala, dada yangu akamwambia “mimi siwezi kulala wewe kama hatujapimwa na virusi vya ukimwi”. Wakanunua zile mashine za kujipima, na walikuwa na pombe na nini, wakaenda kwa chumba cha kulala,” alisimulia.
Kanyari alifichua kuwa ni walipokuwa katika chumba cha kukodisha ambapo mshukiwa aliyemtaja kama muuaji wa mfululizo alipomgeukia dadake.
“Dada yangu hakujua wale ni wauaji. Yeye aliona mtu aliyempenda. Sioni makosa ya dada yangu. Yeye ni mtu ambaye hajaolewa. Alitaka mtu wa kuchumbiana naye. Ni kawaida kila mtu anatafuta mtu wa kuchumbiana naye. Sasa yeye aliona mtu amependa, mtu aliyempenda, akaamua kwenda naye bila kujua yule ni muuaji nay eye sio wa kwanza,” alisema.
Kanyari alisema mwendo wa saa nane usiku, Bi Wahu alijaribu kumpigia simu lakini hakupokea simu.
Alisema kuwa mshukiwa aliendelea kudai shilingi nusu milioni kutoka kwake na kumtishia kabla ya mapigano kuzuka baada ya marehemu kuanza kuwa na upinzani. Ni baada ya Wahu kuanza upinzani ambapo mshukiwa alidaiwa kumdunga kisu mguuni na goti.
“Dada yangu anakuwanga kichwa ngumu. Wakaanza kubishana na kupigana. Katika kupigana, akamdunga kisu ya mguu na shingo. Alafu akatoka na akafunga na kifuli. Dada yangu sasa akang’ang’ana kutoka na hana hoja. Alikufaa hapo kwa mlango akijaribu kung’ang’ana kutoka aende hospitali akatengezwe mguu na shingo,” alisimulia Kanyari.