“Kwani uko na watoto wangapi!” Hisia mseto huku Khalwale akimsherehekea bintiye aliyepita KCSE 2023

Katika miaka ya hivi majuzi, seneta huyo amekuwa na mtahiniwa katika takriban kila KCPE na KCSE inayofanywa.

Muhtasari

•Mwanasiasa huyo wa UDA alimsherehekea bintiye Gift Atubukha Khalwale baada ya kufaulu kupata alama ya B+ katika KCPE 2023.

•Wengi wakionekana kushangazwa na hatua ya maseneta wa kuwa na watahiniwa wa takriban mitihani ya kitaifa ya kila mwaka.

amemsherehekea bintiye Gift Khalwale
Seneta Boni Khalwale amemsherehekea bintiye Gift Khalwale
Image: TWITTER// BONI MTETEZI

Wakenya kwenye mitandao ya kijamii wameendelea kufanya mzaha baada ya seneta wa Kakamega Boni Khalwale kumsherehekea mtoto wake mwingine ambaye alifanya vyema katika mtihani wa KCSE wa mwaka jana.

Katika akaunti yake ya X, mwanasiasa huyo wa UDA alimsherehekea bintiye Gift Atubukha Khalwale baada ya kufaulu kupata alama ya B+ katika KCSE 2023.

Gift ambaye alikuwa mwanafunzi wa shule ya upili ya St Brigids Kiminini alikuwa miongoni mwa wanafunzi takriban laki tisa waliopokea matokeo yao Jumatatu asubuhi.

“Hongera sana, Gift Atubukha Khalwale! Ninataka kushukuru familia yangu, udugu wote wa Shule ya Upili ya St Brigids-Kiminini, na zaidi ya yote, Mungu kwa kumsaidia mdogo wangu Gift kufikia hatua hii muhimu,” Khalwale alisema kwenye tweet.

Seneta huyo zaidi alishiriki matokeo yote ya bintiye ambaye alikuwa amepata alama nzuri katika masomo yote. Alipata B katika Kiingereza, Kiswahili na Biolojia, B- katika Hisabati, C katika Fizikia, B+ katika Kemia, A katika Historia na A- katika CRE.

Kufuatia hayo, Wakenya walimiminika chini ya posti ya Khalwale huku wengi wakionekana kushangazwa na hatua ya maseneta wa kuwa na watahiniwa wa takriban mitihani ya kitaifa ya kila mwaka. Katika miaka ya hivi majuzi, mwanasiasa huyo amekuwa na mtahiniwa katika takriban kila KCPE na KCSE inayofanywa.

Tazama maoni ya baadhi ya Wakenya kwenye Twitter:

Ndegz: Yesu! Hii inaisha lini?

Mr Beast: Anawakilisha kila mwaka bila kukosa.

A Kareem: Kwa kiwango hiki utahitaji tu kura kutoka kwa watoto wako ili kushinda.

Kenya West: Ninamtangaza rasmi Mshauri wangu @KBonimtetezi kuwa baba wa Taifa

John Wambua: Mwanaume amekuwa akisimamisha mgombeaji kila mwaka kwa miaka 24 iliyopita.

Josh: Wewe kwani uko na watoto wangapi Bwana?