Sonko afanya jaribio la tatu kumuokoa Conjestina baada ya kushtumiwa kwa kumtumia vibaya

Aliweka wazi kuwa hii ni mara yake ya mwisho kumsaidia bondia huyo wa zamani ambaye hajakuwa sawa kwa muda.

Muhtasari

•Sonko amejitolea kwa mara ya tatu kumsaidia bingwa wa zamani wa ndondi wa Kenya Conjestina Achieng’ kupata afueni yake.

•Hivi majuzi aliazimika kujitetea baada ya baadhi ya Wakenya kumushutumu kwa kumtumia Conjestina vibaya

ya maktaba ya Mike Sonko na Conjestina ndani ya ndege.
Picha ya maktaba ya Mike Sonko na Conjestina ndani ya ndege.

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko amejitolea kwa mara ya tatu kumsaidia bingwa wa zamani wa ndondi wa Kenya Conjestina Achieng’ kupata afueni yake.

Katika taarifa yake ya Jumanne asubuhi, mwanasiasa huyo alifichua kuwa kupitia usaidizi wake, Conjestina amelazwa tena katika kituo cha kurekebisha tabia cha wanawake cha Mombasa ambapo ataanza matibabu yake upya chini ya uangalizi maalum wa wataalamu.

Hata hivyo, aliweka wazi kuwa hii ni mara yake ya mwisho kumsaidia bondia huyo wa zamani ambaye hajakuwa sawa kwa muda baada ya majaribio yake mawili ya awali ya kutaka kumsaidia kupata nafuu kushindikana.

"Ingawa nafasi yetu katika safari ya uponyaji ya Conjestina ilikatizwa, mimi ni mtu ambaye hakati tamaa maishani. Ni kwa sababu hii kwamba tumempa Conjestina nafasi ya tatu na ya mwisho tena kuhusu kesi yake.

Ningependa tu kujulisha umma kwamba alirudishwa katika kituo cha kurekebisha tabia cha wanawake cha Mombasa ambapo ataanza matibabu yake upya chini ya uangalizi wa kikundi cha wataalamu, wakiwemo washauri, na madaktari wa viungo,” Mike Sonko alisema kupitia Twitter.

Aliambatanisha taarifa yake na video na picha ya bingwa huyo wa zamani wa ndondi akichukuliwa tena katika kituo cha Mombasa Rehabilitation Centre.

“Shukrani zangu za kipekee ziwaendee wasimamizi wa Hospitali ya Wanawake ya Mombasa wakiongozwa na msimamizi mkuu, Mhe. Amina Abdalla kwa kutukubalia tena kituoni. Mungu mbele,” alisema.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya gavana huyo wa zamani kulazimika kujitetea hadharani baada ya baadhi ya Wakenya kumkosoa kwenye mitandao ya kijamii wakimushtumu kwa kumtumia Conjestina vibaya kwa manufaa yake binafsi.

Wakati akijitetea dhidi ya madai hayo wiki jana, mfanyibiashara huyo alitoa ushahidi wa juhudi nyingi alizoweka katika kumsaidia Conjestina na akashutumu familia yake kwa kukatiza juhudi zake.

“Wakenya, nilijitahidi kumsaidia Conjee, lakini familia yake ilipunguza juhudi zangu. Kwa bahati nzuri, moyo wangu ni mkubwa kuliko mimi mwenyewe,” Sonko alisema kwenye taarifa.

Licha ya kusema juhudi zake zilikatizwa, Sonko hata hivyo alidokeza kuwa atafanya jaribio la mwisho la kumsaidia bingwa huyo wa zamani wa ndondi.

“Wakati fulani nashindwa kujizuia kwa upendo nilionao kwa watu hasa wasio na uwezo, na nadhani ndiyo sababu nilimpa Conjee la nafasi ya kwanza, ya pili, na sasa huenda nitalazimika kutoa nafasi ya tatu na ya mwisho tena kwa sababu siku zote huwa niko serious na kesi zote tunazochukua na kwa vile huwa tunaandika na kutoa hesabu kwa maendeleo ya kesi zetu zote nyeti,” alisema.

Sonko aliambatanisha taarifa yake na sauti ambazo alidai ni rekodi za mazungumzo ya simu aliyokuwa nayo na familia ya Conjee alipokuwa akijaribu kufuatilia hali ya bondia huyo wa zamani.