logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Murang'a: Polisi ashambuliwa na genge hatari na kulazimishwa kuvuta misokoto 2 ya bangi

Alisema mabishano ya wanachama wa genge hilo na polisi yaligeuka kuwa mabaya.

image
na Radio Jambo

Habari03 February 2024 - 06:26

Muhtasari


• Alisema mabishano ya wanachama wa genge hilo na polisi yaligeuka kuwa mabaya.

• Inadaiwa maafisa wawili walifanikiwa kujiondoa katika eneo la tukio lakini mmoja huyo aliandamwa na kushurutishwa avute bangi kwa lazima.

Afisa mmoja wa polisi katika kaunti ya Murang’a amelazwa hospitalini katika hali ya kutojielewa baada ya kushambuliwa na genge la majambazi ambalo lilimshrutisha kuvuta hadi misokoto miwili ya bangi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya kustaajabisha iliyochapishwa na Taifa Leo, polisi huyo alikuwa na wenzake wawili ambao walikwenda kufanya msako katika kitongoji kimoja kinachojulikana sana kwa ulanguzi wa dawa za kulevya.

Walipofika na kuwakabili walanguzi hao, polisi hao walilemewa na wawili wakafanikiwa kutoroka huku wakimuacha mwenzao nyuma ambaye aliwekwa mateka na genge hilo na kulazimishwa kuvuta bangi.

“Genge hilo lilidai kwamba hata dakika 20 hazikuwa zimepita tangu polisi wengine wafike hapo na kuchukua hongo,” akasema mhudumu wa bodaboda aliyeshuhudia kisa hicho.

Alisema mabishano ya wanachama wa genge hilo na polisi yaligeuka kuwa mabaya.

Inadaiwa maafisa wawili walifanikiwa kujiondoa katika eneo la tukio lakini mmoja huyo aliandamwa na kushurutishwa avute bangi kwa lazima.

Ripoti ambayo kituo cha polisi cha Murang’a kiliandaa kuhusu kisa hicho ilisema afisa huyo alishambuliwa na watu ambao hawajulikani.

“Tulipata ripoti kwamba kulikuwa na makabiliano kati ya vijana katika kundi mojawapo mtaani na polisi waliokuwa wamevalia kiraia,” ikasema ripoti ya polisi kama ilivyonukuliwa na Taifa Leo.

Iliongeza kwamba maafisa walitumwa eneo hilo na ndipo “mwanamume aliyetambuliwa kuwa ni polisi wa cheo cha konstebo alipatikana akiwa amepoteza fahamu walioshuhudia wakisema kwamba alishurutishwa kuvuta kinachoaminika ni bangi”.

Afisa huyo alikimbizwa katika hospitali ambapo kwa sasa amelazwa akitibiwa athari za kuzimia chini ya shinikizo za ulevi kupindukia.

Kamanda wa Polisi Murang’a Mashariki Mary Wakuu alisema kisa hicho kinachunguzwa na msako utafanywa kunasa washukiwa.

Bi Wakuu alisema mtaa huo wa Kayole kwa muda umekuwa katika darubini ya maafisa wa usalama kutokana na ulanguzi wa mihadarati.

“Ni mtaa ambao lazima tutausafisha. Pia natoa onyo kwa polisi wawe wa kutekeleza busara na uadilifu kazini. Hayo mambo yote yatachunguzwa na taswira kamili itaandaliwa ripoti,” akasema Bi Wakuu.

Alisema watachunguza ikiwa polisi hao watatu nao walikuwa wakiitisha hongo jinsi ilivyodaiwa.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved