Rais Ruto alazimika kuendelea na hotuba gizani baada ya stima kupotea akiongea (video)

Lakini kama hiyo haikuwa aibu tosha kutoka kwa kampuni ya umeme KPLC, rais tena alilazimika kumaliza hotuba yake gizani baada ya stima kupotea akikaribia kuhitimisha.

Muhtasari

• Katika video ambayo ilinaswa katika mkutano huo, Ruto alisikika akiongea kutoka gizani huku akiuliza nni kinaendelea, dakika chache kabla ya umeme kurudi tena.

Rais Ruto gizani
Rais Ruto gizani
Image: screengrab//NTV KENYA

Jumatano wakati wa kilele cha mkutano wa wajumbe wa serikali huko Naivasha, rais Ruto alilazimika kuendelea na maongezi yake gizani baada umeme kupotea kwa takribani mara mbili huku rais akiendelea na hotuba.

Katika video ambayo ilinaswa katika mkutano huo, Ruto alisikika akiongea kutoka gizani huku akiuliza nni kinaendelea, dakika chache kabla ya umeme kurudi tena.

Ruto alikuwa akiwahutubia wajumbe wa Baraza lake la Mawaziri kuhusu ni kwa nini aliwafanya kuwa chaguo lake katika serikali wakati taa zilizimika kwa angalau sekunde tano. Mkuu wa nchi alijaribu kuzungumza kupitia kwa kipaza sauti kwa muda kabla ya taa kuwasha tena.

"Tupo...Oh, sawa," Ruto alisema huku akijaribu kipaza sauti.

Lakini kama hiyo haikuwa aibu tosha kutoka kwa kampuni ya umeme KPLC, rais tena alilazimika kumaliza hotuba yake gizani baada ya stima kupotea akikaribia kuhitimisha.

Itakumbukwa katika siku za hivi karibuni, KPLC imekuwa ikikumbwa na kuyumba kwa mitambo yake ya kuzalisha umeme na kulitumbukiza taifa katika giza kwa saa kadhaa.

Hatua hii imeona baadhi ya watu wakitoa wito kwa rais kumsimamisha kazi waziri wa Kawi Davis Chirchir kwa kile wanahisi ni kuzembea kazini.