Nimedhulumiwa na UDA kwa msimamo wangu wa kisiasa - Wamuchomba

Akizungumza Jumatano, Wamuchomba alisema hii ni kwa sababu ya msimamo wake wa kisiasa kuhusu hali ya mambo nchini.

Muhtasari
  • Kulingana naye, Wakenya wengi hawaelewi ni kwa nini ana tabia tofauti na huchukua misimamo mikali dhidi ya baadhi ya masuala.
  • Mbunge huyo aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha UDA amekuwa akikosoa sera za utawala huo, ambazo anasisitiza zimekuwa zikiwaumiza wananchi.
Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba
Image: SCREENGRAB

Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba sasa anadai kuwa amedhulumiwa na chama chake cha United Democratic Alliance (UDA).

Akizungumza Jumatano, Wamuchomba alisema hii ni kwa sababu ya msimamo wake wa kisiasa kuhusu hali ya mambo nchini.

Mbunge huyo alisema hajawahi kuona haya kusema yaliyo yake na jambo hilo limepelekea chama tawala kufikia hatua ya kutuma wanasiasa wengine kwenda kukabiliana naye, katika jimbo lake.

Mimi husema mawazo ya akili yangu. Nimeonewa vya kutosha. Ikiwa kuna yeyote ambaye amedhulumiwa kwa msimamo wake wa kisiasa katika nchi hii ni Gathoni Wamuchomba na mtendaji, na chama tawala.

"Nimedhulumiwa kiasi cha watu kuja eneo bunge langu kunipigania kisiasa mbele ya watu. Watu wangu wa Githunguri wanajua ninachozungumzia," Wamuchomba alisema.

Mbunge huyo aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha UDA amekuwa akikosoa sera za utawala huo, ambazo anasisitiza zimekuwa zikiwaumiza wananchi.

Hata hivyo, akizungumza na gazeti la Star siku ya Alhamisi, Katibu Mkuu wa UDA Cleophas Malala alisema chama hicho kinalenga kutimiza ahadi zao za kampeni kwa Wakenya.

Alisema kuwa kujibu kila mbwa 'anayebweka' kutavuruga chama hicho kufanya kazi kwa Wakenya na kutekeleza mpango huo.

"Tunaangazia kutimiza ahadi tulizotoa kwa Wakenya wakati wa kampeni. Kwa hivyo, sitakuwa nikijibu kila 'mbwa anayebweka'. Hili litatufanya tukose kuzingatia lengo," Malala alisema.

Mnamo Januari, Wamuchomba alieleza kuwa amekuwa akipinga vikali sera za Kenya Kwanza kwa sababu aligundua kuwa Kenya Kwanza haikujali masaibu ya wapiga kura wake.

Wamuchomba alisema maoni yake mengi yanatokana na mahali na jinsi alivyolelewa na kusomeshwa. Asili hiyo, alisema, inaathiri vitendo na ushawishi wake zaidi ya matarajio ya kisiasa ya watu wengine.

Mbunge huyo alisema hawezi kuketi nyuma wakati baadhi ya sera zinasukumwa kooni mwa Wakenya.

Kulingana naye, Wakenya wengi hawaelewi ni kwa nini ana tabia tofauti na huchukua misimamo mikali dhidi ya baadhi ya masuala.