“Mungu nipe amani!” Kareh B azungumza dereva wa basi lililomuua mwanawe akifikishwa mahakamani

Akizungumza kabla ya kusikizwa kwa kesi hiyo Alhamisi, Kareh B alimuomboleza mwanawe na kuomba amani kutoka kwa Mungu.

Muhtasari

•Kareh B alimwomba Mungu amani kufuatia kushtakiwa kwa dereva wa basi lililopata ajali iliyomuua mwanawe mnamo Aprili 1, 2024.

•Akiwa mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Winam, DK Mtai, Onyango alikana mashitaka hayo.

wakati wa mazishi ya mwanawe mnamo Aprili 12, 2024.
Kareh B wakati wa mazishi ya mwanawe mnamo Aprili 12, 2024.
Image: FACEBOOK// KAREH B

Malkia wa Mugithi Mary Wangari Gioche almaarufu Kareh B alimwomba Mungu amani kufuatia kushtakiwa kwa dereva wa basi lililopata ajali iliyomuua mwanawe mnamo Aprili 1, 2024.

Wiki jana, Bw George Onyango Riako ambaye alikamatwa siku moja baada ya ajali hiyo alishtakiwa kwa kusababisha kifo cha mwanafunzi mmoja na kuwajeruhi wengine tisa. Aliachiliwa kwa dhamana ya Sh200,000 pesa taslimu au bondi ya Sh500,000.

Huku akizungumza kabla ya kusikizwa kwa kesi hiyo siku ya Alhamisi, Kareh B aliomboleza mwanawe na kuomba amani kutoka kwa Mungu.

"Kwa hivyo, hatimaye dereva wa Chavakali alikamatwa, akafikishwa kortini na kuachiliwa kwa dhamana, chini ya kosa la trafiki. Kusikizwa kwake ni leo .... Mungu nipe Amani,” Kareh B alisema kupitia Facebook siku ya Alhamisi asubuhi.

Bw Onyango alishtakiwa katika Mahakama ya Sheria ya Winam mnamo Aprili 18, siku chache tu baada ya mwanawe  Kareh B,  Joseph Mwadulo kuzikwa katika kaunti ya Embu.

Karatasi ya mashtaka ilionyesha kuwa mshukiwa aliendesha gari lililokuwa limebeba wanafunzi wa Shule ya Upili ya Wavulana ya Chavakali kwa mwendo wa kasi sana.

Ilisema namna alivyoendesha gari hilo ni hatari kwa umma kwa kuzingatia hali zote ikiwa ni pamoja na asili, hali na matumizi ya barabara na wingi wa magari kwa wakati huo au yanayotarajiwa kuwa barabarani.

Inasemekana alitumia breki ngumu kwa makusudi wakati akikaribia mzunguko wa Coptic na hivyo kupoteza udhibiti wa gari na kusababisha kuyumba upande wa kushoto kabla ya kutua upande huo huo wa basi na kumuua mmoja.

Akiwa mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Winam, DK Mtai, Onyango alikana mashitaka hayo.

Mtai alimwachilia kwa dhamana ya Sh200,000 pesa taslimu au bondi ya Sh500,000.

Aliagiza kuwa kesi hiyo kutajwa leo,  Aprili 25, 2024.