“Msipige vita waganga, wana umuhimu wao pia!” Rais Museveni aiomba kanisa

Museveni alisema kwamba waganga wa jadi walikuwa na nafasi yao tena kubwa tu katika kufanikisha ushindi wa vita vya msituni vilivyopelekea yeye kuanzisha serikali mapema miaka ya 80s.

Muhtasari

• Ingawa alitoka katika familia ya kidini, Museveni alisema alifanya kazi kwa karibu na waganga wa kienyeji na mara nyingi alifuata mwongozo wao wakati wote wa vita vya msituni.

• "Ilinibidi kutafuta njia za kuwashawishi na kufanya kazi nao bila kuwahukumu kama vile ninavyosikia vikundi vingine vikiwahukumu," alisema.

Museveni
Museveni
Image: X

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amewataka viongozi wa dini na viongozi wengine wa serikali kuacha kuwatenga watu wanaofanya uganga na dini za kimila.

Museveni alisema alisikitishwa kwamba baadhi ya viongozi wa makanisa mara nyingi hujihusisha na makabiliano na wanamila, bila kutambua jinsi wanavyoweza kuwa muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Rais Museveni aliyasema hayo Jumapili, Juni 9 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mashujaa Kitaifa yaliyofanyika Wilayani Gomba.

"Ninapokuwa Kampala, wakati mwingine ninasikia viongozi wa makanisa wakishambulia dini za jadi ambazo zina nguvu sana katika maeneo kama haya," Museveni alisema.

"Hata hivyo, ni hawa (wana mila) ambao walitusaidia katika vita vilivyoleta serikali hii. Vijana waliokuwa wakiendesha bunduki zetu walitoka katika nyumba zenye asili ya kitamaduni.”

Badala ya kukabiliana na waganga, Museveni alisema viongozi wa kidini na serikali wanapaswa kuwatendea kama alivyofanya wakati akiwaamuru waasi wa NRA miaka ya 1980.

Ingawa alitoka katika familia ya kidini, Museveni alisema alifanya kazi kwa karibu na waganga wa kienyeji na mara nyingi alifuata mwongozo wao wakati wote wa vita vya msituni.

"Ilinibidi kutafuta njia za kuwashawishi na kufanya kazi nao bila kuwahukumu kama vile ninavyosikia vikundi vingine vikiwahukumu," alisema.

"Niliwahimiza tu kutekeleza matambiko yao, huku tukituruhusu kutekeleza jukumu letu. Niliwaongoza waziwazi kuhusu kazi zilizohitaji sayansi, bunduki za mashine na chokaa. Wangeweza kusali kwa miungu yao itusaidie tulipokuwa tukiendesha bunduki hizo.”

Museveni alisimulia mganga mmoja kama huyo aitwaye Mpiima, ambaye angewaambia wakae kwa saa nyingi na kumsubiri awaroge wanajeshi wa serikali, na walitii.

Katika tukio moja, alisema, alifanywa kuruka juu ya mzoga wa kuku kama moja ya ibada.

Hata hivyo, Museveni anasema alifanya kazi kwa karibu na makundi ya kidini pia.

Kwa mfano, anakumbuka kusherehekea Siku ya Krismasi ya 1982 katika Kanisa Katoliki la Kasana na pia kufanya maombi na makasisi wa Kianglikana na Duwas pamoja na Maimamu.

"Ushauri wangu kwenu viongozi wa dini, muwe na subira na kubadilishana mawazo na sio kuamrisha watu tu," alisema.

Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa mwaka huu nchini Uganda yalifanyika chini ya kaulimbiu; “Tuwasalimie Mashujaa Wetu; Uganda salama sasa ni Ukweli.”

Tazama otuba yake hapa kuanzia saa 2.12.13