Shirika la habari la Nation limetangaza kurejea kwa kipindi cha uchekeshaji cha Churchill Show kwenye runinga ya NTV, ikiwa ni miaka miwili tangu kipindi hicho kilipogura NTV.
Churchill Show, kipindi kinachoongozwa na ‘baba’ wa tasnia ya kisasa ya burudani za vichekesho, Daniel Ndambuki maarufu kama Churchill kiliondoka NTV miaka miwili iliyopita kwenda shirika la habari la Cape Media, runingani TV47.
Hata hivyo, Churchill Show haikuweza kudumu kwa muda mrefu hewani kwani baadae iliingia chini ya maji na ni furaha kwa mashabiki wa vichekesho baada ya kutangazwa kurudi mahali kilipoasisiwa, NTV.
Wakitangaza taarifa hizo, NTV walisema kwamba ni uamuzi uliosukumwa Zaidi na mashabiki ambao kwa muda wamekuwa wakitaka Churchill Show kurudishwa hewani.
“Subiri imekwisha, Kenya! Kipindi maarufu cha #ChurchillShow🔥 kinajirudi baada ya miaka mingi ya maombi kutoka kwenu, mashabiki! Tulikusikia kwa sauti na wazi, na tunakuletea vichekesho vilivyogawanyika kando, na michoro ya kufurahisha unayopenda. 💯 Jitayarishe kwa msimu mpya wa burudani safi! Endelea KUFUATILIA,” NTV Kenya walitaarifu kupitia ukurasa wao wa Facebook.
Kipindi cha ucheshi cha Churchill Show kilikwenda hewani NTV kwa mara ya kwanza mwaka 2007 na kufikia kikomo Mei 2022.
Katika kipindi hicho, Daniel Ndambuki aliwajenga wachekeshaji kadhaa ambao wengi wao ni maarufu mpaka sasa, hivyo kujidhihirisha kama mmoja wa mihimili mikuu katika tasnia ya ucheshi humu nchini.
Bila shaka, kurejea kwa shoo hiyo katika runinga hiyo ya kitaifa kutakuwa kama mwamko mpya kwa tasnia ya ucheshi ambayo imeonekana kujikwaa na kusalia sakafuni katika miaka ya hivi karibuni tangu janga la Corona.