Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa amejiteua na kujitangaza kama mwenyekiti wa vuguvugu la vijana wa Gen Z.
Kupitia ukurasa wake wa X, Barasa alisema kwamba aliamua kuchukua hatua hiyo baada ya vijana hao kuonekana kutokuwa na kiongozi na hata kusisitiza kwamba hawana haja ya kuwa na uongozi ili matakwa yao kusikilizwa.
Barasa alisema kwamba yeyote atakayejaribu kupinga hilo atatembelewa na vijana kwa ‘salamu’ ambayo ni kutafuta namba yake na kuiweka bayana mitandaoni kwa watu umpigia simu na kumtumia jumbe.
Pia mbunge huyo wa UDA alitangaza kuwa yuko mbioni kumtafuta makamu wake.
“Leo nimejiteua kuwa mwenyekiti wa Gen Z. Sasa nahitaji Makamu mwenyekiti....kuanzia sasa Gen Z wasiseme hawana kiongozi tena. Mwenye anasena ngoooo...tunaenda kumusalimia ile salamu yetu,” Barasa aliandika.
Hata hivyo, wengi walimkumbusha kwamba Gen Z hawana uongozi na wala hawana haja ya kujigawanya kwa misingi ya ukabila.
Tangazo la Barasa linakuja siku mbili baada ya rais Ruto kuomba Gen Z kuwasilisha majina ya wawakilishi 2 wa jinsia yoyote kwa kamati itakayoundwa kushughulikia masuala ibuka nchini.
Makataa ya kuwasilishwa kwa majina kutoka vikundi mbalimbali ni Julai 7.