Waziri Murkomen akiri kuwa na saa ya 900k, kiatu cha 80k, mshipi wa 50k, suti ya 30k, tai ya 20k

Kipchumba Murkomen amekiri kuwa na udhaifu wa kupenda sana vitu kadhaa za bei ghali.

Muhtasari

•Seneta huyo wa zamani wa kaunti ya Elgeyo Marakwet alifunguka kuhusu baadhi ya nguo na vitu zvya bei ghali alizo nazo.

•Alibainisha kuwa amesikia ukosoaji kutoka kwa Wakenya wakilalamikia mtindo wake wa maisha ghali na kuweka wazi kuwa yuko tayari kubadilika.

Image: FACEBOOK// KIPCHUMBA MURKOMEN

Waziri wa Barabara na Uchukuzi, Onesmus Kipchumba Murkomen, amekiri kuwa na udhaifu wa kupenda sana mavazi kadhaa ya bei ghali.

Katika mahojiano kwenye Obinna TV Extra, seneta huyo wa zamani wa Elgeyo Marakwet alifunguka kuhusu baadhi ya mavazi na vitu vya bei ghali alizo nazo.

"Kiatu changu cha gharama kubwa kinaweza kuwa elfu 70-80, mshipi ni karibu elfu 40-50. Lakini sihitaji kuvaa mishipi miwili kwa miaka miwili, mshipi mmoja unatosha,” Murkomen alisema.

Alishauri kwamba mtu kuwa na mshipi wa gharama kubwa, na wa ubora wa hali ya juu unaoweza kupinduliwa na kuonekana tofauti ni bora kwani unaweza kutumika kwa muda mrefu.

Waziri huyo pia alikiri kuwahi kununua saa ya bei ghali ya takriban Ksh900,000, suti za takriban Ksh20,0000-30,000, na tai ya takriban Sh20,000.

“Ukinunua saa yenye thamani ya 900,000, unaivaa kwa miaka ishirini. Hutakaa ukisema, mwezi ujao nanunua saa nyingine. Ukinunua kiatu kizuri, unavaa miaka miwili.

Ukinunua mshipi nzuri ya kupindua, unavaa hiyo miaka miwili na bado unang’ara tu. Alafu unatafuta tai nzuri inang’aa ya 15,000-20,000 unasurvive nayo,” alisema.

Seneta huyo wa zamani hata hivyo alibainisha kuwa amesikia ukosoaji kutoka kwa baadhi ya Wakenya wakilalamikia mtindo wake wa maisha ghali na kuweka wazi kuwa yuko tayari kubadilika.

“Ninashukuru maoni ambayo yamekuja kutoka kwa Wakenya kuhoji ni kwa nini nimevaa saa ya bei ghali, au kiatu cha bei ghali. Na ni kweli, kama ningechukua pesa hizi labda kuwekeza kwenye soko la pesa kununua kitu kwa bondi, labda zingeniletea faida na kuendelea kufanya kitu kingine. Ikiwa ningetumia pesa hizo labda kupanua shamba langu la parachichi, labda ningepata dola chache kwa kuuza parachichi hizo,” Murkomen alisema.

Aliongeza, “Kwa kweli nataka kuwaambia Wakenya ambao wamenikosoa kwa kuvaa saa hizo kwamba huo ni udhaifu wangu, lakini niko tayari kujirekebisha. Iwapo saa au aina fulani ya viatu vitawafanya watu ninaowahudumia kuvuruga umakini wao kutoka kwa mambo muhimu ambayo ni lazima niwajibishwe kwayo, na pengine kugeuza usikivu wa raia au mwanafamilia. Nimewaambia marafiki zangu, hiyo saa inaweza kukaa.

Murkomen ni miongoni mwa maafisa wakuu wa serikali ambao wameshutumiwa hadharani katika siku za hivi majuzi kutokana na mtindo wao wa maisha ghali.

Wakenya wamedai uwajibikaji miongoni mwa wafanyikazi wa umma na kuwataka wakome kabisa kuonyesha maisha ya kifahari hadharani.