"Rais sio mjuaji!" Kuria amjibu vikali Oparanya baada ya kutishia kujiuzulu kama waziri

Huku akijibu matamshi ya Oparanya, waziri wa zamani Moses Kuria alimweleza wazi kuwa rais sio mjuaji.

Muhtasari

•Kuria amemjibu vikali waziri Wycliffe Oparanya baada ya kutishia kujiuzulu kutoka kwa baraza la mawaziri la rais William Ruto.

•Oparanya alibainisha kuwa yuko tayari kufanya kazi katika serikali ya Kenya Kwanza iwapo tu hawatajifanya kuwa wanayajua yote.

amemjibu waziri Wycliffe Oparanya.
Moses Kuria amemjibu waziri Wycliffe Oparanya.
Image: HISANI

Aliyekuwa waziri wa utumishi wa umma, utendakazi na usimamizi wa uwasilishaji kazi, Moses Kuria amemjibu vikali waziri Wycliffe Oparanya baada ya kutishia kujiuzulu kutoka kwa baraza la mawaziri la rais William Ruto iwapo mapendekezo yake hayatatekelezwa.

Akizungumza wakati wa Ibada ya Kanisa moja siku ya Jumapili, Oparanya alibainisha kuwa serikali inayoongozwa na William Ruto ilimtafuta ikitaka awasaidie katika utawala wa nchi.

Aliweka wazi kuwa yuko tayari kuisaidia serikali lakini kwa masharti ya kwamba inazingatia  mikakati anayopendekeza.

“Hawa wameangalia, wakaangalia, wameona huyu mzee anaweza kusaidia kazi. Nitawasaidia, lakini nikiwaambia tuende njia hii na wanakataa, mimi nitajiondoa, na nirudi kwangu,” alisema.

Gavana huyo wa zamani wa kaunti ya Kakamega alibainisha kuwa yuko tayari kufanya kazi katika serikali ya Kenya Kwanza iwapo tu hawatajifanya kuwa wanayajua yote.

Aidha, mwanasiasa huyo mkongwe alibainisha kwamba ni lazima mtu akubali kusaidiwa kila anapoomba msaada.

“Lazima ukubali kusaidiwa. Lakini tukiwa hapo na wewe alafu unajifanya mjuaji, tutakuwa na shida,” alisema.

Huku akijibu matamshi ya Oparanya siku ya Jumatatu, waziri wa zamani Moses Kuria alimweleza wazi kuwa rais sio mjuaji.

"Mpendwa Ambetsa, rais wangu si mjuaji," Kuria aliambia Oparanya kupitia mtandao wa Twitter.

Hisia za Oparanya zinakuja siku chache tu baada ya yeye, na mawaziri wengine kumi na wanane kuapishwa katika wizara tofauti.

Kwa upande wake, Moses Kuria hakurejeshwa katika baraza la mawaziri la serikali ya Kenya Kwanza baada ya yeye na mawaziri wengine wote waliohudumu katika baraza la mawaziri la hapo awali kufutwa mapema mwezi uliopita. Wenzake kadhaa walirejeshwa katika baraza jipya la mawaziri lakini aliachwa nje.