Oscar Sudi kumnunua Nuru Okanga nyumba Nairobi na kumpa Sh1.3M kuanzisha biashara

"Nenda tafuta nyumba Kibera ama Mukuru kwa Njenga, hizi zinajengwa sasa hivi. Tafuta nyumba ya vyumba vya kulala 3, nitakununulia kama nimenunulia watoto,” Sudi alimwambia Okanga.

Muhtasari

• Sudi kwa upande wake, alikubali kumpa hela hizo lakini akaongeza kwamba angependa kumnunulia nyumba jijini Nairobi ili kumrahisishia maisha yake.

OKANGA NA SUDI
OKANGA NA SUDI
Image: HISANI

Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi ametoa ahadi ya kubadilisha kabisa maisha ya mwanasiasa Nuru Okanga.

Akizungumza kwenye kipindi cha Obinna ambapo walikutana wote wawili, Sudi alimtaka Okanga kujieleza kwa uwazi ni kipi ambacho angependa mbunge huyo mkwasi kumfanyia.

Okanga alianza kwa kuomba angalau 300k kwa ajili ya kumfungulia mkewe biashara ya ususi naye akajiombea Sh1m kwa ajili kufungua carwash, duka na ‘kisiagi’.

“Niko na familia kila mtu anajua, na nimeoa msomi, anajua kusuka lakini pesa ya kumuanzishia biashara ndio sina. Nikipata kama 300k saluni yote itakuwa imekamilika, hiyo ni kwake, nimweke busy,” Okanga alisema.

“Sasa tukija kwa mimi kama Nuru Okanga, ile familia nimetoka mimi ndio kama tegemeo la kila mtu. Mwenyewe sina kazi, shida zangu nikieleza zote ni nyingi lakini nataka niende kwa moja mahsusi. Mheshimiwa kwa roho nzuri yako Mungu akuingie, kama unaweza nipatie Sh1m, biashara yangu itakuwa sawa kabisa.”

“Nitaenda niweke biashara yangu na nitulie, nyumbani kwetu mahali nimezaliwa hakuna kisiagi, nitanunua kisiagi niweke hapo. Hapo kwetu hakuna duka karibu, hivyo nitaweka duka na pia nitaweka biashara ya mambo ya kutengeneza fenicha na eneo la kuoshea magari na pikipiki,” aliongeza.

Sudi kwa upande wake, alikubali kumpa hela hizo lakini akaongeza kwamba angependa kumnunulia nyumba jijini Nairobi ili kumrahisishia maisha yake.

“Mimi nitakupa hizo pesa, unipatie akaunti nikuwekee hizo pesa. Lakini pia kando na hiyo fanya hivi, nenda tafuta nyumba Kibera ama Mukuru kwa Njenga, hizi zinajengwa sasa hivi. Tafuta nyumba ya vyumba vya kulala 3, nitakununulia kama nimenunulia watoto,” Sudi alisema.