DP Gachagua aomba kanisa kuondoa marufuku ya wanasiasa kuhutubu kanisani (video)

“Unajua sasa mwanasiasa akiona kipaza sauti na aone watu wameketi na hawezi wahutubia, huwa anahisi vibaya. Lakini wenyewe ndio tuliharibu, tumekubali makosa yetu." Gachagua alisema

Muhtasari

• Kwa mujibu wa Gachagua, mwanasiasa yeyote anahisi vibaya sana kuona kipaza sauti mbele yake na umati mkubwa wa waumini bila kupewa nafasi hata kidogo ya kuwahutubia.

GACHAGUA
GACHAGUA
Image: FACEBOOK

Naibu wa rais Rigathi Gachagua ametoa ombi kwa kanisa kuondoa marufuku ya wanasiasa kuhutubu kanisani.

Akizungumza katika Parokia ya Mtakatifu Joseph wa Arimathea katika Dayosisi ya Nairobi mnamo Jumapili, Agosti 25, Gachagua alipendekeza kuwa kutokuwepo kwa mazungumzo ya kisiasa kanisani huenda kukasababisha mtafaruku kuhusu masuala ya kitaifa.

Kiongozi huyo aliwaomba viongozi wa kanisa kuwapa ruhusu wanasiasa kuwahutubia waumini ambao pia ni wapiga kura katika maeneo ya ibada.

Kwa mujibu wa Gachagua, mwanasiasa yeyote anahisi vibaya sana kuona kipaza sauti mbele yake na umati mkubwa wa waumini bila kupewa nafasi hata kidogo ya kuwahutubia.

“Tukienda kuleta maneno mingi kanisani tunaambiwa siku hizi hakuna. Sasa tutakaa namna hiyo. Lakini Askofu mkuu utuangalie mwaka huu kuelekea mwisho wa mwaka unaweza kurejelea, hivyo kama sisi ambao tunapewa nafasi ya kuzungumza kwa niaba yao tutaonyesha adabu, mwape nafasi tu,” Gachagua alisema.

“Unajua sasa mwanasiasa akiona kipaza sauti na aone watu wameketi na hawezi wahutubia, huwa anahisi vibaya. Lakini wenyewe ndio tuliharibu, tumekubali makosa yetu. Tulileta mambo mingi kanisani yale hayafai; mpaka matusi, chuki, kuongea vibaya… na nafikiri ni sahihi wakati tunakuja kanisani kwa ajili ya kuabudu tu,” Naibu rais aliongeza.

Viongozi katika maeneo mengi ya kuabudu walipiga marufuku hotuba za kisiasa kanisani haswa baada ya vijana wa Gen Z kutoa onyo kali kwa makanisa.

Takwa hili liliona viongozi wengi wa kanisa wakiingiwa na woga dhidi ya kukubalia wanasiasa kuhutubia kanisani.