Kifaranga wa 'ndege hatari zaidi duniani' aanguliwa

Kumekuwa na visa vya watu kuuawa na cassowary, cha hivi karibuni zaidi mnamo 2019.

Muhtasari

•Kifaranga huyo ni wa nne kuanguliwa barani Ulaya mwaka huu na mzaliwa wa kwanza nchini Uingereza tangu 2021.

•"Tulipomuona kifaranga huyo kwa mara ya kwanza tulifurahi sana," mlinzi Alistair Keen alisema.

Image: BBC

Kifaranga wa cassowary, mojawapo ya ndege wakubwa na hatari zaidi duniani, ameanguliwa kwa mara ya kwanza katika mbuga ya ndege ya Cotswolds kusini magharibi mwa England.

Wafugaji katika hifadhi ya Birdland mjini Gloucestershire, wamekuwa wakijaribu kufuga ndege wakubwa, wasioweza kuruka kwa zaidi ya miaka 25.

Kifaranga huyo ni wa nne kuanguliwa barani Ulaya mwaka huu na mzaliwa wa kwanza nchini Uingereza tangu 2021.

"Tulipomuona kifaranga huyo kwa mara ya kwanza tulifurahi sana," mlinzi Alistair Keen alisema.

"Cassowary wana sifa ya kuwa mojawapo ya ndege hatari zaidi duniani na ukubwa wao, kasi na nguvu pamoja na makucha yao kama kisu, cha ukubwa wa10cm inamaanisha kuwa tunapaswa kuwatunza kwa uangalifu mkubwa.

Cassowary, ambaye anahusishwa na misitu ya asili ya kitropiki huko New Guinea na kaskazini mwa Australia, anachukuliwa kuwa hatari sana kwa sababu ya miguu yake yenye nguvu, makucha makali na mkali anapotishiwa.

Kumekuwa na visa vya watu kuuawa na cassowary, cha hivi karibuni zaidi mnamo 2019, wakati Marvin Hajos, 75, alipofariki baada ya kushambuliwa na mmoja wa cassowary wake.