Kebaso awarai wasanii kuimba kuhusu uongozi mbaya na ufisadi na si kuimba mapenzi na pombe

“Ninataka kuzungumza na wanamuziki wote nchini Kenya, Mapinduzi yote katika historia yalichochewa na kazi za sanaa na muziki. Hatutaki kusikia nyimbo za mapenzi, kuachana, dawa za kulevya, majambazi n.k"

Muhtasari

• “Wakati wa maandamano ya GenZ mlifanya vizuri. Hasa kuonekana mitaani na kutumbuiza kwenye matamasha. Lakini baada ya hapo mmenyamaza. ," Kebaso alisema.

MORARA KEBASO SNR
MORARA KEBASO SNR
Image: FACEBOOK

Mwanaharakati wa kutoa elimu ya kiraia, Morara Kebaso ametoa rai kwa wasanii wa humu nchini kufikiria kuhusu kutunga nyimbo za kukashifu ufisadi na uongozi mbaya.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Kebaso alisema kwamba kwa sasa kila Mkenya anataka kusikia kitu chochote kinachonyoosha kidole kwa uongozi mbaya wa serikali na ufisadi iliokithiri na hivyo kuwataka wasanii kutumia fursa hiyo vizuri.

Aliwaomba wasanii kukoma kuimba kuhusu masuala ya mapenzi na pombe, ambayo imekuwa kama kawaida kwa tungo nyingi za miaka ya hivi karibuni, na badala yake kuimba kuhusu uanaharakati na mabadiliko.

“Ninataka kuzungumza na wanamuziki wote nchini Kenya, Mapinduzi yote katika historia yalichochewa na kazi za sanaa na muziki. Hatutaki kusikia nyimbo za mapenzi, kuachana, dawa za kulevya, majambazi n.k. Hiyo sio hisia zetu. Mnahitaji kuanza kuchukua jukumu kubwa katika mapinduzi,” alirai.

Akitlea mfano wa mchekeshaji Crazy Kennar ambaye hivi majuzi alifanya video ya kuchekesha inayoonyesha ufisadi serikalini na ambayo ilivutia wengi, aliwarai wasanii pia kufanya hivyo kama njia moja pia ya kuuza Sanaa yao kwa Wakenya.

“Umegundua kuwa hivi sasa ni ngumu sana kutoa wimbo mzuri kama sio juu ya utawala mbaya na ufisadi? Ndiyo. Hali ya taifa ni kwamba tunahitaji mabadiliko. Crazy Kennar alifanya video hivi karibuni na ina views Milioni 46 kwenye instagram pekee. Kwa sababu ilihusu rushwa na utawala mbovu. Ni wakati wako wa kuendana na hali ya taifa,” alisema.

Hata hivyo, aliwapa maua yao wasanii kwa kujitokeza wakati wa maandamano ya Gen Z na kufanya vyema kwa kutumia Sanaa yao mitaani na kuwataka kurejesha moto uo huo.

“Wakati wa maandamano ya GenZ mlifanya vizuri. Hasa kuonekana mitaani na kutumbuiza kwenye matamasha. Lakini baada ya hapo mmenyamaza. Tuambie mmesimama wapi. Je, mnacheza salama? Je, mna huzuni na hali ya taifa? Je, mnasubiri mood ibadilike?” aliwauliza wasanii.