Mwanamke mwenye umri wa miaka 27 akamatwa na polisi kwa kumla paka

Kamera zilimuonyesha akimkanyaga paka kichwa na kumuua kabla ya kuanza kumla. Alipatikana na manyoya kwenye midomo yake pamoja na damu kwenye mikono.

Muhtasari

• "Maafisa waliweza kubaini kwamba Allexis alikuwa amevunja kichwa cha paka kwa mguu wake na kisha kuanza kumla paka huyo," polisi waliandika katika ripoti yao.

Mwanamke aliyefungwa jela pingu mikononi.
Mwanamke aliyefungwa jela pingu mikononi.
Image: Shutterstock

Mwanamke mmoja ametiwa mbaroni na maafisa wa polisi baada ya kunaswa kwenye kamera za siri akimla paka.

Kwa mujibu wa ripoti kutoka jimbo la Ohio nchini Marekani, Allexis Ferrell mwenye umri wa miaka 27 alinaswa kwenye kamera za siri akimkanyaga paka kichwani na kumuua kabla ya kumla mnyama huyo na wakati wa kukamatwa, alipatikana na manyonya kwenye midomo yake pamoja na damu mikononi.

Ferrell ni mzaliwa wa mji huo, ulio umbali wa maili 172 kutoka Springfield - ambapo madai ambayo hayajathibitishwa kwamba wahamiaji wa Haiti 'wanakula wanyama wa kipenzi' yamezua kashfa ya kitaifa.

Ingawa yeye si mhamiaji wala si kutoka Springfield, video ya kukamatwa kwake imesambazwa mtandaoni katika mijadala na blogu kuhusu suala hilo. 

Mamlaka sasa imefichua video ya kamera ya tukio hilo.

"Maafisa waliweza kubaini kwamba Allexis alikuwa amevunja kichwa cha paka kwa mguu wake na kisha kuanza kumla paka huyo," polisi waliandika katika ripoti yao kwa mujibu wa vyombo vya habari Marekani.

Inakuja baada ya Donald Trump kutoa madai ya ajabu na ambayo hayajathibitishwa wakati wa mjadala wake wa urais kwamba wahamiaji wa Haiti wanaua na kula wanyama wa kipenzi wa majirani zao huko Springfield.