Quiver Kilimani: Klabu ya kwanza Nairobi kuburudisha wateja bila muziki

Klabu hiyo sasa inasema kwamba kwa kuondoa muziki wa sauti kubwa, wageni bado wanaweza kula, kunywa, na kujiburudisha huku wakishiriki mazungumzo yenye maana zaidi.

Muhtasari

• Klabu hiyo sasa inasema kwamba kwa kuondoa muziki wa sauti kubwa, wageni bado wanaweza kula, kunywa, na kujiburudisha huku wakishiriki mazungumzo yenye maana zaidi.

QUIVER KILIMANI KUHUDUMU BILA MUZIKI.
QUIVER KILIMANI KUHUDUMU BILA MUZIKI.
Image: FACEBOOK//QUIVER-KILIMANI

Uongozi wa klabu ya Quiver, tawi la mtaa wa kifahari wa Kilimani umejibu taarifa za kutishiwa kufngwa na mamlaka kutoka kaunti ya Nairobi kutokana na malalamishi ya majirani kwamba klabu hiyo inawapa usumbufu wa kelele.

Katika barua ambayo ilionekana na meza yetu ya habari, Quiver walitangaza kuanzisha mkakati wa kupata suluhu kwa tatizo hilo la kelele kwa majirani wake katika mtaa wa Kilimani.

Quiver walitangaza kwamba wameamua kukumbatia mkakati wa kuwaburudisha na kuwahudumia wateja wao bila kuwepo kwa muziki, hatua mabayo itakuwa kama suluhu la kudumu kwa kero ya kelele katika mtaa huo.

"Kufuatia maendeleo ya sasa kulingana na maoni ya ujirani wetu na roho ya umoja, uhifadhi wa mazingira, na mazungumzo mengi ya simu kati ya majirani zetu wazuri na wasimamizi wetu, tunataka kuleta uamuzi huu wa msingi kwa umma: tutakuwa klabu ya kwanza kukumbatia dhana ya kibunifu kwa kutocheza muziki,” sehemu ya taarifa hiyo ilisoma.

Klabu hiyo sasa inasema kwamba kwa kuondoa muziki wa sauti kubwa, wageni bado wanaweza kula, kunywa, na kujiburudisha huku wakishiriki mazungumzo yenye maana zaidi.

"Mtazamo wetu wa kipekee unalenga kuunda nafasi ambapo wageni wanaweza kufurahia wakati wao kikamilifu bila usumbufu wa muziki wa sauti kubwa. Tunaamini watu bado wanaweza kuwa na wakati mzuri wa kuungana, kushiriki katika furaha ya umoja," Quivers alisema.

Uongozi wa klabu ulihakikisha kuwa wafanyakazi wake waliojitolea watapatikana ili kuhakikisha wageni wanahisi kukaribishwa na kuburudishwa.

"Tunapoanza safari hii mpya, tunakaribisha kila mtu kujiunga nasi. Kwa pamoja, tunaweza kuunda mazingira ya amani na yanayofaa, yasiyo na kelele, ambapo nishati ya wageni wetu huweka sauti ya jioni.”

Haya yanajiri baada ya afisa wa kaunti anayesimamia mazingira, Geoffrey Mosiria kuzuru eneo hilo siku chache zilizopita na kusema huenda watalazimika kuwapokonya leseni kutokana na malalamishi ya majirani wake.

"Imetubidi tufunge biashara kwa sababu walipuuza arifa nyingi na malalamiko kutoka kwa majirani. Tabia hii ni kinyume cha sheria, na sasa tunatekeleza hatua dhidi ya wale ambao wameshindwa kushughulikia maombi yetu ya kuzuia sauti. Hatuwezi kuruhusu uchafuzi wa mazingira unaoendelea na usumbufu kwa amani ya jamii yetu,” alisema Mosiria.