Boniface Mwangi afichua sababu maalum kwa nini huwa anawabusu watoto wake kila siku

Ujumbe huu unajiri siku chache tu baada ya mwanaharakati huyo kufunguka kuhusu jinsi nusura ajitoe uhai.

Muhtasari

•Mwangi alizungumzia jinsi anavyoonyesha upendo kwa watoto wake kila siku akijua kuwa inaweza kuwa yangu ya mwisho.

•Aliambatanisha ujumbe wake na picha nzuri yake akiwa Nalia.

Mwanaharakati Boniface Mwangi na binti yake Nalia
Image: X//BONIFACE MWANGI

Mwanaharakati na mwandishi maarufu wa Kenya Boniface Mwangi amemsherehekea binti yake Naila Mwangi anapoadhimisha miaka 14 ya kuzaliwa kwake.

Katika taarifa ya kusherehekea bintiye, Mwangi alizungumzia jinsi anavyoonyesha upendo kwa watoto wake kila siku akijua kuwa inaweza kuwa yangu ya mwisho.

"Leo ni siku ya kuzaliwa ya binti yangu. Naila anafikisha miaka 14. Mimi huwabusu watoto wangu kila siku, nikijua inaweza kuwa yangu ya mwisho,” Mwangi alisema.

Aliambatanisha ujumbe wake na picha nzuri yake akiwa Nalia.

Ujumbe huu unajiri siku chache tu baada ya mwanaharakati huyo kufunguka kuhusu jinsi nusura ajitoe uhai  mapema mwezi uliopita kufuatia masuala aliyokuwa akipitia.

Kupitia ujumbe mrefu aliouchapisha kwenye  X, Mwangi ambaye alikuwa mstari wa mbele kuongoza maandamano ya kupinga serikali ya rais Ruto alisema kwamba alijikuta katika kiza kinene ambapo chaguo pekee akilini mwake lilikuwa ni kujitoa uhai.

Mpiga picha huyo wa zamani alifichua kwamba alikuwa anamaanisha uamuzi wake huo, kiasi kwamba alikuwa tayari ameandika wosia wake na hata kuwapigia simu ya mwisho baadhi ya watu wake wa karibu.

“Mnamo Agosti 3, 2024, nilijipata mahali penye giza sana na nikafikiria kujiua. Siku chache mapema, nilikuwa nimetia saini wosia wangu, kisha nikapiga simu au kutuma ujumbe mfupi kwa watu wachache. Ilikuwa ni kuaga kwangu. Nilitaka kufa. Ondoka kwenye ulimwengu huu kwa wema,” alisema.

Mwangi alisema kwamba fikira ya kutaka kujiondoa duniani mwenyewe zilisukumwa na matukio ambayo yalikuwa yamejiri nchini kwa wakati huo – kuona umwagikaji wa damu wa vijana waliokuwa wanaandamana.

“Kulikuwa na maumivu mengi sana, huzuni, na kiwewe maishani mwangu hivi kwamba sikuweza kustahimili tena. Sikuweza kuendelea kutazama bila msaada huku nchi yetu ilipokuwa ikiingizwa katika mzozo mbaya wa ghasia zilizoidhinishwa na Serikali, zikilenga Wakenya wasio na hatia,alifunguka.

Hata hivyo, hakuweza kufanikisha fikira zake kwani familia yake ilimfika karibu na kumpa msaada mkuu wa kumtafutia matibabu na ushauri nasaha wa kiakili.