DJ Brownskin alituma video ya mkewe akinywa sumu kwa mpenzi wake mwingine- DCI

Idara ya DCI imesema mcheza santuri huyo atashtakiwa kwa kosa la kusaidia kujitoa uhai na kushindwa kuzuia kitendo hicho.

Muhtasari

•DCI walisema mcheza santuri huyo alikamatwa siku ya  Alhamisi kuhusiana na kifo cha mkewe Sharon Njeri.

•Wapelelezi wamebaini kuwa baada ya kurekodi video hiyo, Brownskin aliituma kwa mpenzi wake mwingine anayeishi nje ya nchi.

amekamatwa kuhusiana na kifo cha mkewe Sharon Njeri
DJ Brownskin amekamatwa kuhusiana na kifo cha mkewe Sharon Njeri
Image: HISANI

Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) imethibitisha kukamatwa kwa mcheza santuri Michael Macharia Njiiri almaarufu DJ Brownskin.

Katika taarifa ya Jumapili, DCI walisema mcheza santuri huyo alikamatwa siku ya  Alhamisi kuhusiana na kifo cha mkewe Sharon Njeri.

Idara hiyo ilieleza kwamba Brownskin alikamatwa baada ya kukaidi agizo la kujisalimisha kwa polisi ili kutoa maelezo zaidi kuhusu kifo cha mkewe ambaye aliaga dunia baada ya kudaiwa kunywa sumu mwezi Julai mwaka jana.

"Katika kanda ya video ya kuhuzunisha moyo iliyotolewa na mwanablogu maarufu mnamo Aprili 1, miezi 9 baada ya mwili wa Njeri kuzikwa, dakika zake za mwisho zilirekodiwa na DJ akimimina sumu kwenye kikombe na kumeza bila kusita.

Kisha alijilaza kwenye kochi na kuwaita watoto wake wawili kuwajulisha kuhusu kifo chake kinachokaribia. Mama huyo wa watoto wawili alianguka na kufariki muda mfupi baadaye. Alizikwa nyumbani kwa wazazi wake katika kijiji cha Koimbe Weithaga, Kaunti ya Murang’a, Agosti 6 mwaka jana," taarifa ya DCI ilisoma.

Taarifa hiyo iliendelea kufichua kwamba wapelelezi wameweza kubaini kuwa baada ya kurekodi video ya mkewe akinywa sumu, Brownskin aliituma kwa mpenzi wake mwingine anayeishi nje ya nchi.

"Juhudi za kumwita mshukiwa ili kutoa mwanga zaidi kuhusiana na tukio hilo hazikufua dafu, kwani alijificha na kuwafanya wapelelezi kuanzisha msako mkali uliopelekea kukamatwa kwake siku ya Madaraka Day, baada ya saa sita usiku," taarifa ilisoma.

DCI imethibitisha kwamba mshukiwa anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kasarani ambapo anaendelea kuhojiwa kabla ya kushtakiwa.

"Atashtakiwa kwa kosa la kusaidia kujitoa uhai na kushindwa kuzuia hilo kinyume na Kifungu cha 225 (C) cha Kanuni ya Adhabu."

Mkewe DJ Brownskin, Sharon Njeri alifariki usiku wa Julai 29 na Julai 30 baada ya kudaiwa kunywa sumu nyumbani kwao Nairobi.

Njeri alizikwa Agosti 6 nyumbani kwa wazazi wake Murang'a na mshukiwa ni miongoni mwa waombolezaji waliohudhuria maziko.