DJ Fatxo hatimaye afunguka kuhusu uhusiano wake na Jeff Mwathi aliyefariki nyumbani kwake

Mwimbaji huyo alisema alijuana na Jeff kwa takriban miaka miwili na hata walifanya biashara pamoja.

Muhtasari

•"Nimemjua Jeff kwa miaka miwili. Alikuwa akiniuzia viatu. Nimenunua jozi nyingi za viatu kutoka kwa Jeff tangu mwaka wa 2021," Fatxo alisema.

•Fatxo alidai kuwa hakuwa nyumbani kwake wakati kijana huyo alipotoweka. Alisema alikuwa amemwacha marehemu na wenzake wawili.

Marehemu Jeff Mwathi na DJ Fatxo
Image: HISANI

Mwimbaji wa Mugithi Lawrence Njuguna almaarufu DJ Fatxo hatimaye ameeleza upande wake kuhusu kifo cha kutatanisha cha kijana wa miaka 23, Geoffrey Mwathi almaarufu Jeff ambaye alipatikana amefariki nyumbani kwake Kasarani, Nairobi.

Jeff alifariki mnamo Februari 22 baada ya kudaiwa kujitoa uhai kwa kuruka kutoka nyumba ya DJ  Fatxo iliyo katika orofa ya kumi ya jumba la Redwood Apartments kwenye barabara kuu ya Thika. Msanii huyo tangu wakati huo amewekwa katikati ya kifo hicho chenye utata ikizingatiwa kuwa kijana huyo alifariki nyumbani kwake.

Akizungumza na Wanahabari siku ya Jumapili,  DJ Fatxo ambaye katika siku za hivi majuzi amekabiliwa na ghadhabu kubwa kutoka kwa Wakenya wenye uchungu mwingi alifichua kuwa marehemu alikuwa rafiki yake. Alisema alijuana na Jeff kwa takriban miaka miwili na hata walifanya biashara pamoja.

"Nimemjua Jeff kwa miaka miwili. Alikuwa akiniuzia viatu. Nimenunua jozi nyingi za viatu kutoka kwa Jeff tangu mwaka wa 2021," alisema.

Mwimbaji huyo kutoka kaunti ya Nyandarua alisimulia jinsi alivyotembelea duka la Jeff na kupenda jinsi alivyokuwa amelipamba na hata kueleza nia ya kutafuta huduma zake endapo angewahi  kuhitaji kupamba duka lake. 

Fatxo alidai kuwa hakuwa nyumbani kwake wakati kijana huyo alipotoweka. Alisema alikuwa amemwacha marehemu na wenzake wawili.

"Nilitoka na wanawake watatu. Baadaye kurudi baada ya masaa kadhaa niligundua kuwa Jeff hakuwa ndani ya nyumba na wengine walikuwa, mimi ndiye nilienda na wao kwa kituo cha polisi kuripoti kuwa Jeff ametoweka," alisema.

Mwanamuziki huyo maarufu alisema kuwa yeye ndiye aliyefichua habari za kifo cha Jeff kwa familia yake. Alisema alikuwa tayari kushirikiana na familia kumzika rafikiye huyo lakini kwa bahati mbaya hawakuwa wakimjibu.

"Nilifikia hatua ya kumuomba mama yangu awasiliane na familia yake ili wakubali tushirikiane kwa sababu hili lilikuwa jambo geni kwangu. Hakuna jinsi ningeweza kupoteza rafiki na nikose kumwomboleza," alisema.

Aidha, aliweka wazi kwamba yuko tayari kushirikiana na wapelelezi na kudai kwamba pia yeye anatafuta majibu.