Lilian Ng'ang'a ashinda mzozo wa hisa dhidi ya aliyekuwa mumewe Gavana Mutua

Lilian anamiliki 50% ya hisa katika Ndash Enterprises Ltd.

Muhtasari

• Lilian alisema hisa zake 1800 katika Ndash Enterprises  Ltd zilirejeshwa kufuatia malalamiko aliyotoa Novemba 2021.

•Kando na hisa, Lilian pia alimshtumu Mutua kwa kuchukua gari iliyokuwa imeandikishwa kwa jina lake.

Gavana Mutua na aliyekuwa mkewe Lilian Nganga
Gavana Mutua na aliyekuwa mkewe Lilian Nganga
Image: INSTAGRAM//GOVERNOR ALFRED MUTUA

Lilian Nganga ni mtu mwenye furaha baada ya msajili wa kampuni kumrejesha hisa zake alizodai zilichukuliwa na dadake aliyekuwa mumewe Alfred Mutua.

Katika taarifa aliyotoa Jumatatu, Lilian alisema hisa zake 1800 katika Ndash Enterprises  Ltd zilirejeshwa kufuatia malalamiko aliyotoa Novemba 2021.

"Baada ya uchunguzi wa kina kuhusu uhamisho wa hisa 1800, Msajili wa Makampuni mnamo tarehe 6/5/2022 alipata umuhimu wa malalamiko ya Bi Nganga na amerejelea rekodi katika kampuni na uhamisho laghai wa hisa 1,800," Taarifa iliyotiwa saini na wakili wa Lilian, Philip Murgor ilisoma.

Mwaka jana Lilian alimshtumu Mutua kwa kutumia njia haramu kuchukua hisa zake 1800 na kuzihamisha kwa dadake Ann Mutua baada ya kutengana kwao.

Taarifa ya Lilian imeonyesha kila mmoja wao ana hisa 50%  katika Ndash Enterprises, kampuni  inayomiliki mkahawa wa A&L.

Kando na hisa, Lilian pia alimshtumu Mutua kwa kuchukua gari iliyokuwa imeandikishwa kwa jina lake.

"Bwana Mutua ameguswa sana na kutengana kwetu. Ingawa nilisema nataka kusonga mbele na maisha yangu, alifikiria vingine" Lilian amesema.

Mke huyo wa sasa wa Juliani alidai kuwa Mutua alitishia kuchukua kila kitu anachomiliki na kumsababishia mahangaiko tele maishani.

Pia alisema mume huyo wake wa zamani alimwagiza arejeshe pesa na mali yote alizowahi kumpatia walipokuwa pamoja.

"Mutua anatazamia kunidhulumu kisaikolojia na kiuchumi na lazima serikali imzuie!!" Alisema.

Mwezi Novemba mahakama ilitupilia mbali ombi la Mutua la kutaka kesi yake na Lilian kuhusu umiliki wa mali ihamishwe kutoka Nairobi hadi Machakos.