Miguna Miguna avunja kimya kuhusu mchango wa kurejea kwake unaoendelea

Wakili huyo alifichua kuwa ametumia zaidi ya milioni tatu katika majaribio kya kurud iKenya.

Muhtasari

•Wakili huyo aliyefurushwa amesema kuwa mpango huo ni wa kweli wala sio udanganyifu kama ilivyodaiwa.

•Miguna litangaza kuwa  atatua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) asubuhi, Oktoba 20, 2022.

Tangazo la kuchangisha pesa kwa ajili ya kurejea kwa Miguna Miguna
Image: TWITTER//

Wakili Miguna Miguna amevunja ukimya wake  kuhusu mpango unaoendelea wa kuchangisha pesa kwa ajili ya kurejea kwake nchini.

Kupitia akaunti yake ya Twitter, wakili huyo aliyefurushwa amesema kuwa mpango huo ni wa kweli wala sio udanganyifu kama ilivyodaiwa.

"Wao si wadanganyifu. Ni Wakenya waaminifu wanaojaribu kuchangisha pesa kihalali kutoka kwa wale walio tayari kutoa BURE ili kunipa mapokezi ya nyumbani wanayopanga,"  alimjibu mtumizi wa Twitter aliyehoji uhalisi wa mpango huo.

Mwanamitandao huyo alikuwa akiuliza kuhusu bango la kuchangisha pesa ambalo limekuwa likisambazwa kwenye mitandao ya kijamii lililoandikwa  "Jenerali Miguna Miguna Arejea Nyumbani', "Haki ya Miguna ni Haki kwa Wakenya wote."

Mshauri wa kisiasa huyo wa zamani wa Raila Odinga alibainisha kuwa yeye hujihusisha tu na watu waadilifu.

"Huu ni uadilifu," alisema.

Hapo awali Miguna alifichua kuwa ametumia zaidi ya milioni tatu katika majaribio kya kurudi nyumbani  nyakati tofauti.

Alisema itakuwa haki kuwaruhusu wafuasi wake kumsaidia huku akidokeza kuwa watu wengi wangefanya  hivyo ikiwa wangekuwa katika nafasi yake.

“Huwezi kusema vivyo hivyo ikiwa nyumba yako ingeharibiwa vibaya na vilipuzi vilivyolipuliwa na Wahuni wa Serikali, uliteswa, ukazuiliwa kinyume cha sheria kisha kulazimishwa kutoka katika nchi yako ya kuzaliwa kwa miaka mitano, na umetumia zaidi ya dola 30,000 za pesa zako kujaribu kurejea nyumbani,” alisema.

Mwezi uliopita wakili huyo anayeishi Canada  alitangaza kuwa  atatua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) asubuhi, Oktoba 20, 2022.

Awali alikuwa amesema kwamba atarejea nchini tarehe 25 Oktoba kabla ya kubadilisha tena tarehe ya kurejea Kenya. 

"Ratiba ya kurudi nyumbani. Baada ya takriban miaka 5 ya uhamisho wa kulazimishwa, ninarudi nyumbani. Kuondoka Toronto: Oktoba 24, 2022. Nitawasili JKIA, Nairobi: Oktoba 25, 2022, saa mbili na dakika 20 usiku. Tutaonana, na kila mtu, " alisema.

Kabla ya hayo alikuwa amedai kuwa amepokea pasipoti mpya huku akimpongeza Rais William Ruto kwa kufanikisha hilo.