Nabii Kanyari avunja kimya kuhusu kwa nini dada yake, Scarlet Wahu alizikwa haraka

“Jumamosi saa mbili tulimzika tukiwa watu ishirini peke yake. Na hiyo mazishi ikaisha maana hatukutaka aibu," Kanyari alisema.

Muhtasari

•Kanyari alithibitisha kuwa familia ilimzika marehemu Wahu Jumamosi, Januari 6, siku mbili tu baada ya mwili wake kupatikana.

•Kanyari alifichua kuwa maandalizi yote ya maziko yalifanywa siku ya Ijumaa baada ya dadake kuuawa Alhamisi usiku.

Nabii Victor Kanyari amesimulia kuhusu kifo cha dada yake Starlet Wahu
Image: HISANI

Mchungaji mwenye utata wa Kenya, Nabii Victor Kanyari, hatimaye amezungumza kuhusu mazishi ya marehemu dada yake, Starlet Wahu na kueleza ni kwa nini alizikwa kwa haraka.

Wakati akiwahutubia waumini katika kanisa lake siku ya Jumapili, mtumishi huyo wa Mungu anayeongoza kanisa la Salvation Healing Ministry alithibitisha kwamba familia yake ilimzika marehemu Wahu siku ya Jumamosi, Januari 6, siku mbili tu baada ya mwili wake kupatikana katika chumba cha kukodi cha AirBnB katika mtaa wa South B, jijini Nairobi.

Alifichua kuwa aliishauri familia yake kumzika haraka kwani hakutaka usumbufu wa vyombo vya habari kuhusiana na suala hilo la kusikitisha.

“Dada yangu alidungwa kisu na akafariki hapo hapo. Wakati alipofariki papo hapo, hakukuwa na jambo lingine ila kumzika,” Kanyari alisimulia.

Aliendelea, “Mimi niliambia familia, tumzike haraka kwa sababu sitaki watu wa media wanisumbue. Kwa kusema Kanyari, Kanyari, Kanyari, eti dada ya Kanyari. Sasa nikaona watanisumbua nikaambia mama yangu maana amekufa na hatafufuka, tumzike.”

Kasisi huyo mwenye utata alifichua kwamba maandalizi yote ya maziko yalifanywa siku ya Ijumaa baada ya dadake kuuawa Alhamisi usiku.

“Jumamosi saa mbili tulimzika tukiwa watu ishirini peke yake. Na hiyo mazishi ikaisha maana hatukutaka aibu. Hata hatutaka mchango. Hata wale ambao walikuwa wakinitumia mchango, nilikuwa nareverse,” alisema.

Alisema kuwa yeye binafsi ndiye aliyeshughulikia gharama zote za mazishi kwani hakutaka msaada wowote kumzika mdogo wake.

Katika hotuba yake, Kanyari alisisitiza kuwa dadake alijuana na muuaji wake kupitia mitandao ya kijamii na wawili hao wakakutana kujiburudisha.

“Ni kweli dada yangu alipata mwanaume na yule mwanaume akamchumbia mitandaoni. Na wakati alimdate katika mitandao, wakapendania huko kwa Facebook. Wakati walipendana yule mwanaume akamwalika akamwambia kuja tukule na tukunywe. Mwanaume akamwambia yeye ni tajiri sana, na wasichana wa siku hizi wanapenda matajiri,” Prophet Kanyari alisimulia.

Alibainisha kuwa dadake alikuwa mwanasosholaiti na alikuwa na wafuasi wengi sana kwenye mitandao ya kijamii.

“Sasa yule mwanaume akamuita. Wakaenda kwa klabu fulani wakakula nyama, wakakunywa pombe. Walipomaliza kula nyama na kunywa pombe, yule mwanaume akamwambia basi ningetaka tuwe na urafiki.

Wakakubaliana. Na wakakodisha nyumba ya kwenda kulala. Wakati wa kulala, dada yangu akamwambia “mimi siwezi kulala wewe kama hatujapimwa na virusi vya ukimwi”. Wakanunua zile mashine za kujipima, na walikuwa na pombe na nini, wakaenda kwa chumba cha kulala,” alisimulia.

Kanyari alifichua kuwa ni walipokuwa katika chumba cha kukodisha ambapo mshukiwa aliyemtaja kama muuaji wa mfululizo alipomgeukia dadake.

“Dada yangu hakujua wale ni wauaji. Yeye aliona mtu aliyempenda. Sioni makosa ya dada yangu. Yeye ni mtu ambaye hajaolewa. Alitaka mtu wa kuchumbiana naye. Ni kawaida kila mtu anatafuta mtu wa kuchumbiana naye. Sasa yeye aliona mtu amependa, mtu aliyempenda, akaamua kwenda naye bila kujua yule ni muuaji nay eye sio wa kwanza,” alisema.

Kanyari alisema mwendo wa saa nane usiku, Bi Wahu alijaribu kumpigia simu lakini hakupokea simu.