Watu 10 wafariki, 11 wajeruhiwa katika ajali kwenye barabara kuu ya Nairobi-Mombasa

Ajali hiyo ilitokea Jumatatu, Aprili 1 usiku baada ya matatu hiyo kugongana ana kwa ana na lori lililokuwa likija, polisi na walioshuhudia walisema.

Muhtasari
  • Uokoaji ulitatizwa vibaya na mvua iliyokuwa ikinyesha katika eneo hilo wakati huo, maafisa walisema.
Tukio la ajali katika Barabara Kuu ya Nairobi - Mombasa eneo la Mlima Kiu huko Mukaa, Kaunti ya Makueni mnamo Aprili 1, 2024.
Tukio la ajali katika Barabara Kuu ya Nairobi - Mombasa eneo la Mlima Kiu huko Mukaa, Kaunti ya Makueni mnamo Aprili 1, 2024.
Image: HISANI

Takriban abiria kumi wamefariki na wengine 11 kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari mawili ya abiria na lori katika eneo la Salama, kwenye barabara kuu ya Mombasa Road.

Mgongano huo ulihusisha matatu mbili na trela.

Waliofariki ni pamoja na watoto wawili wa kike wenye umri kati ya miaka mitano na minane, kijana wa kiume mwenye umri wa takriban miaka mitano, watu wazima watatu wa kike na wanne wa kiume.

Ajali hiyo ilitokea Jumatatu, Aprili 1 usiku baada ya matatu hiyo kugongana ana kwa ana na lori lililokuwa likija, polisi na walioshuhudia walisema.

Polisi walisema ajali hiyo ilitokea katika eneo la Mlima Kiu na kuhusisha matatu zilizokuwa zikielekea Nairobi.

Walioshuhudia walisema kuwa dereva wa lori inasemekana alikosa kufuata njia yake ifaayo ya trafiki na pia aligeuka kulia ghafla na bila tahadhari na hivyo kugongana ana kwa ana na matatu kutoka kwa saccos mbili za eneo hilo.

Ajali hiyo pia iliathiri gari la saloon lililokuwa eneo la tukio.

Abiria wanne waliuawa papo hapo huku wengine wakifariki kutokana na majeraha hospitalini, polisi walisema.

Abiria 4 waliokuwa kwenye magari tofauti wanahofiwa kufariki huku wengine wakijeruhiwa vibaya na wamekimbizwa katika hospitali ya Sultan Hamud.

Waliojeruhiwa walikimbizwa katika hospitali ya Sultan Hamud wakiwa na majeraha mengi.

Uokoaji ulitatizwa vibaya na mvua iliyokuwa ikinyesha katika eneo hilo wakati huo, maafisa walisema.

Miili hiyo ilihamishwa hadi katika hifadhi ya maiti ya eneo hilo ikisubiri kutambuliwa na kufanyiwa uchunguzi.

Ajali hiyo iliathiri mtiririko wa magari katika barabara kuu yenye shughuli nyingi kwa zaidi ya saa mbili kabla ya kuwasili kwa uimarishaji zaidi ili kusaidia katika kudhibiti hali hiyo.

Barabara kuu inadaiwa kuwa mojawapo ya zinazoongoza kwa ajali.

Haya yanajiri huku kukiwa na kampeni inayoendelea ya kukabiliana na ongezeko la visa vya ajali nchini.

Polisi na maafisa kutoka Mamlaka ya Kitaifa ya Usafiri na Usalama wanashiriki katika kampeni ya kukabiliana na tishio hilo barabarani.

Zaidi ya watu 1,000 wamepoteza maisha katika ajali za barabarani tangu Januari mwaka huu.