KRA yanasa bidhaa gushi Mombasa zenye thamani ya shs. milioni 5

Muhtasari

•Bidhaa zilikuwa na chapa feki za KRA.

•Bidhaa za maji na pombe zilinaswa.

Bidhaa bandia zilizonaswa Mombasa
Bidhaa bandia zilizonaswa Mombasa

Oparesheni ya mamlaka ya ukusanyaji ushuru nchini KRA siku ya Jumatano ilipelekea kunaswa kwa bidhaa gushi zenye thamani ya shilingi milioni tano zilizokuwa na chapa bandia za KRA katika kaunti ya Mombasa.

Katika taarifa siku ya Ijumaa KRA ilisema kwamba oparesheni hiyo iliyotekelezwa baada ya kupokea vidokezo kutoka kwa wananchi iliwanasa washukiwa kadhaa katika maduka ya Sliquor stores eneo la Nyali Centre, Simple Life Trading, Minasota Traders Limited zote katika eneo Bombolulu , Coral Limited mtaani Kongowea, Naseem Salim Mohamed trading na Classic Mini Grocers katika eneo la Kongowea miongoni wa wengine.

“KRA ilipokea malalamishi kuhusu ukora wa baadhi ya wafanyibiashara wa kuuza maji ili waepuke kulipa ushuru unaotakikana,” taarifa ya KRA ilisema.   

Bidhaa zilizonaswa na ambazo zinadaiwa kuwa gushi ni maji ya Ahlan ice, Rayan ice purified water, Rehaan ice na Active Sparkle.

Mbali na maji haya bidhaa kadhaa za pombe na sharubati pia zilinaswa katika oparesheni hiyo. Baadhi ya bidhaa zilizonaswa pia ni Piston Premium Vodka, Red star vodka, Bacardi carta blanca, mikebe ya Fever tree tonic na sharubati aina ya  sanpellegrino miongoni mwa bidhaa zingine.

 Kulingana na KRA bidhaa hizo hazikuwa na chapa halali za KRA.

KRA ilimesema kwamba uchunguzi bado unaendelea na washukiwa watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka mbali mbali.

Gari lililokuwa likitumiwa kusafirisha bidhaa hizo pia linazuiliwa.