Kenya yalaani kufurushwa kwa balozi wake nchini Somalia

Muhtasari

• Siku ya Jumapili, serikali ya Somal a ilisema kwamba ilikuwa imemfurusha balozi wa Kenya.

• Mogadishu ilitaja kile ilisema muingilio wa Kenya kwa maswala yake ya ndani na ya kisiasa.

• Katibu wa kudumu Kamau Macharia alisema Nairobi inatathmini hatua ya Mogadishu na itajibu kupitia taratibu zinazostahili.

Rais Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Somalia Mohamed Abdullahi Farmaajo. Picha: MAKTABA
Rais Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Somalia Mohamed Abdullahi Farmaajo. Picha: MAKTABA

Kenya imelaani hatua ya taifa la Somalia kufurusha balozi wa Kenya Lucas Tumbo kutoka nchini humo.

Katibu wa kudumu wa mashauri ya nchi za kigeni Kamau Macharia alielezea masikitiko yake kuhusiana na hatua hiyo ya Jamhuri ya Somalia.

Macharia alisema kwamba Nairobi ilikuwa inatathmini hatua hiyo ya Mogadishu na itajibu kupitia taratibu zinazostahili na kwa wakati unaofaa.

 

 “Hii ni tabia isiyotarajiwa na isiyo na sababu kutoka kwa uongozi wa Somalia, ni jambo ambalo linahitaji kutathminiwa kwanza kabla hatujalizungumzia. Tutajibu rasmi kupitia njia zinazofaa hivi karibuni,” Macharia alisema.

Katika taarifa yake katibu wa kudumu Kamau Macharia alisema kwamba Kenya imewapa makao maelfu ya raia wa Somalia zikiwemo familia za viongozi wa nchi hiyo na hatua ya kufurusha balozi wa Kenya haina msingi wa kutosha.

Alisema raia wa nchi hiyo vile vile wameruhusiwa kumiliki na kuendesha biashara kubwa nchini Kenya bila tatizo lolote.

Siku ya Jumapili, serikali ya Somalia ilisema kwamba ilikuwa imemfurusha balozi wa Kenya Lucas Tumbo na kumuagiza balozi wake mjini Nairobi pia kurejea nyumbani Somalia.

Mogadishu ilitaja kile ilisema muingilio wa Kenya kwa maswala yake ya ndani na ya kisiasa.

"Serikali ya muungano ya Somalia inaelezea masikitiko yake kwa serikali ya Kenya kuhusu  uingiliaji dhahiri wa Kenya katika maswala ya ndani na ya kisiasa ya Somalia ambayo ina uwezo wa kuwa kikwazo kwa uthabiti," ilisema taarifa kutoka kwa wizara ya mambo ya nje ya Somalia.

Huu ni mzozo tu wa hivi punde wa kidiplomasia baina ya nchi hizi mbili za kanda ya Afrika Mashariki huku mzozo mkubwa ukiwa hukusu mpaka katika Bahari Hindi unaozozaniwa na nchi hizi mbili.

 

Hata hivyo Kenya imekuwa ikijihusisha sana na harakati za kuleta amani katika kanda hii na hasa kuimarisha uhusiano wake na taifa la Somalia.

Kenya ni miongoni mwa mataifa katika AMISOM yanayoendelea na harakati za kuangamiza kundi la Kigaidi la Al Shabaab lenye makao yake nchini Somalia na ambalo limetekeleza mashambulizi mengi nchini Kenya na nchini Somalia.