Ruto amjibu Uhuru kuhusu siasa za ukabila

Muhtasari

  • 'Ruto alisema alimwunga mkono Uhuru sio kwa sababu ya kabila lake. 

  • Alisema siasa za ukabila zinarejesha Kenya nyuma.

• Ruto alisema kiongozi wa nchi atachaguliwa kwa sera na sio kulingana na kabila.

 

Naibu rais William Ruto akizungumza katika kanisa la House of Hope mtaani Kayole siku ya Jumapili, Januari 10, 2021.
Naibu rais William Ruto akizungumza katika kanisa la House of Hope mtaani Kayole siku ya Jumapili, Januari 10, 2021.
Image: DPPS

Naibu Rais William Ruto siku ya Jumapili alimkosoa Rais Uhuru Kenyatta kwa kile alitaja kama kurejesha taifa nyuma kwa siasa za ukabila.

Ruto alisema alimsaidia Uhuru mara tatu akijua kwamba alikuwa anatoka jamii ya Wakikuyu na alikuwa mtoto wa Rais wa zamani.

Akizungumza katika Kanisa la ‘House of Hope’ eneo la Kayole siku ya Jumapili, Ruto alisema kiongozi wa nchi atachaguliwa kwa sera na sio kulingana na kabila.

 

Alikashifu wafuasi wa ‘Handshake’ akisema kwamba kuna wengine wanasubiri kupewa urais katika katika mikutano ya bodi na baa.

“Nilimwunga mkono Uhuru sio kwa sababu ya kabila lake. Sikumuunga mkono kwa sababu alikuwa akiwakilisha kabila lake, "Ruto alisema.

Ruto alikuwa akimjibu Rais Kenyatta ambaye alisema siku ya Jumamosi kuwa labda ni wakati wake wa kumuunga mkono mgombea nje ya eneo la Mlima Kenya na jamii ya Wakalenjin.

Uhuru alisema kuwa Kenya imekuwa ikiongozwa na jamii mbili tu tangu uhuru na kwamba huu sasa  unaweza kuwa wakati wa jamii zingine ambazo hazijaonja uongozi wa taifa.

"Ata mimi naweza simama hapa na  niseme kuna jamii tu mbili za Kenya ambazo zimetawala. Labda ni nafasi ya jamii nyengine pia kutawala. Jamii za Kenya ni nyingi," Uhuru alisema.

"Siasa hazipaswi kuegemea misingi ya kikabila lakini kwa itikadi na ajenda zenye busara ambazo zinaweza kuliendeleza taifa hili mbele," Rais alisema.

Rais aliendelea kusema kuwa ‘handshake’ ilikusudia kuunganisha taifa baada ya joto kali la kisiasa ambalo lililetwa na uchaguzi wa 2017.

 

Alisema kwamba mwafaka wake na Raila haukukusudiwa kuzuia wengine kupata nafasi za uongozi.