Mwanafunzi aliyedunga walimu wake visu Kisii aachiliwa kwa dhamana

Muhtasari

  • Mwanafunzi huyo alikanusha mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkaazi Mwandamizi Onchoro.

  • Alishtakiwa kwa kujaribu kuwaua walimu wake wawili katika ofisi za shule hiyo kwa kuwadunga akitumia kisu cha jikoni.

Mwanafunzi wa Shule ya Kisii mwenye umri wa miaka 17 siku ya Jumanne alikanusha mashtaka kujaribu kuua walimu wake wawili katika shule hiyo.

Mwanafunzi huyo alikanusha mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkaazi Mwandamizi Onchoro wakati aliposhtakiwa katika mahakama ya Kisii.

SRM Onchoro alimwachilia mshukiwa kwa dhamana ya Shilingi 100, 000 au dhamana ya pesa taslimu ya Shingi 50, 000 na mdhamini wa kiasi sawa au kupelekwa rumande ya watoto ya Manga Kaunti ya Nyamira kwasababu alikuwa mwanafunzi.

Mwanafunzi huyo ambaye aliwakilishwa na wakili Ben Gichana alishtakiwa kwa kujaribu kuwaua Edward Mokaya na Elvis Maoto katika ofisi za shule hiyo kwa kuwadunga akitumia kisu cha jikoni.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na Hillary Kaino haukupinga kuachiliwa kwa dhamana kwa mwanafunzi huyo.

"Hakuna sababu ya kwetu kupinga kuachiliwa kwake kwa dhamana," Kaino aliiambia korti.

Mwanafunzi huyo alikuwa amevalia sare yake kamili ya shule - sweta ya kijani, shati jeupe na suruali ya kijivu na alionekana kuwa mtulivu wakati wote wa akiwa mahakamani.

Inadaiwa alimshambulia Mokaya kwa kumuadhibu kwa kuchelewa darasani na Maoto kwa kujaribu kumwokoa mwenzake ambaye alikuwa akishambuliwa.

Mokaya ambaye alipata ya kukatwa kichwani amelazwa katika Hospitali ya Ram huko Kisii naye Maoto alitibiwa na kuruhusiwa.

Kesi hiyo itatajwa Januari 27 kabla ya kusikilizwa.