Raila apongeza MCAs kwa kuidhinisha marekebisho ya katiba

Muhtasari

Alisema matokeo hayo yamethibitisha msimamo wake wa mapema kwamba nchi hii imo katika wakati wa kikatiba.

Kinara wa upinzani Raila Odinga
Raila Odinga Kinara wa upinzani Raila Odinga

Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga amewapongeza wakilishi wadi baada ya zaidi ya mabunge 38 ya kaunti kupiga kura kupitisha Muswada wa Marekebisho ya Katiba, 2020.

Kiongozi huyo wa ODM alisema hatua ya mabunge hayo itafanikisha kufanyika kwa kura ya maamuzi, ambayo kulingana na kamati inayosimamia mchakato wa BBI inapaswa kufanyika mwezi Juni mwaka huu.

Katika taarifa kwa vyumba vya habari siku ya Jumanne, Raila ambaye pia ni mjumbe maalum wa AU kuhusu Miundombinu alisema licha ya propaganda na habari potovu ambazo zilikuwa zikienezwa kuhusu mchakato wa mabadiliko ya sheria, mabunge wa kaunti yalisimama kidete.

"Mabunge ya kaunti yameweza kujibu kampeni ya mwaka mzima ya uwongo, habari potovu na ushawishi usiofaa kuhusu BBI na marekebisho ya katiba," Raila alisema.

"Nawashukuru wawakilishi wadi na magavana wetu ambao walikataa kukubali kutokuaminiana, ujinga na kupitisha Muswada huo kwa nguvu."

Alisema matokeo hayo yamethibitisha msimamo wake wa mapema kwamba nchi hii imo katika wakati wa kikatiba.

Kaunti ambazo zimeidhinisha muswada wa marekebisho ya katika 2020
Kaunti ambazo zimeidhinisha muswada wa marekebisho ya katika 2020

“Kama nilivyosema wakati wa uzinduzi wa ukusanyaji wa saini za Muswada huu, nimefanya kazi na watu wetu kwenye michakato ya mabadiliko kama hii kwa muda mrefu. Ninajua kwa kweli kwamba Wakenya sio wanafunzi wepesi linapokuja suala la kutambua wakati wa mabadiliko. ”

Kinara huyo wa upinzaji alibaini kuwa vita sasa vinahamia kwenye bunge la kitaifa na seneti, na kuongeza kuwa nchi inakaribia kura ya maamuzi.

"Tunakaribia kuwapa watu wetu mageuzi wanayohitaji kuunda umoja, utangamano, utulivu na ustawi ambao pia unashughulikia uhalifu wa kiuchumi."

Kufikia sasa mabunge ambayo tayari yameidhinisha muswada huo ni  Siaya, Kisumu, Homa Bay, Migori, Busia, Kakamega, Bungoma, Trans Nzoia, Vihiga, West Pokot, Nakuru, Nairobi, Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga na Kiambu. Wengine ni Meru, Nyamira, Narok, Kajiado, Taita Taveta, Kitui, Makueni, Lamu, Mombasa, Kwale, Garissa, Machakos, Muranga, Samburu, Marsabit na Kisii Ni Bunge la Baringo pekee lililokataa Muswada huo.