Magoha aonya walimu wakuu dhidi ya kuwachanganya watahiniwa

Muhtasari

• Waziri alisema kwamba walimu hao wakuu wamekuwa wakiwachanganya wanafunzi kwa kuwafanya kudurusu karatasi bandia na kukumbana na maswali tofauti.

• Kufikia Jumanne, serikali ilikuwa imechukua zaidi ya vifaa 832 vya kigeni katika vituo vya mitihani ikiwa ni pamoja na simu za rununu na karatasi bandia.

Waziri wa elimu George Magoha amewashauri wasimamizi wa vituo vya kufanyia mtihani kutokuwa walafi na kununua karatasi gushi za mtihani wa KCSE.

Magoha siku ya Jumatano alisema kwamba serikali imegundua kuwa baadhi ya wakuu wa shule ambao ndio mameneja wa vituo vya kufanyia mtihani wamekuwa wakifanya jitihada kushiriki udanganyifu wa mitihani.

Waziri alisema kwamba walimu hao wakuu wamekuwa wakiwachanganya wanafunzi kwa kuwafanya kudurusu karatasi bandia na kukumbana na maswali tofauti wanapoingia katika chumba cha mtihani.

 

Magoha aliwahakikishia wakenya kuwa serikali imejitolea kuhakikisha kwamba mitihani yote inalindwa  na kwamba hakuna karatasi inayovuja.

Kulingana na waziri, hakuna karatasi halisi ya mtihani iliovuja, akisema kwamba tayari wameratibu maeneo ambapo majaribio ya wizi wa mitihani yamekithiri.

"Mitihani imekuwa ikiendelea vizuri kote nchini hadi watu wengine walipoanza kuwachanganya watoto kwa kuwapa karatasi bandia. Wasimamizi wa vituo pia walisambaza karatasi hizo bandia kwenye mtandao," Magoha alisema.

Akizungunza siku ya Jumatano alipoongoza zoezi la kusambaza mitihani mjini Homa Bay waziri alihimiza maafisa wa usalama kutolegeza kamba katika kudumisha usalama wa mitihani.

Wasimamizi wa mitihani walihimizwa kufanya uhakiki kamili na kupiga msasa watahiniwa ili kuwazuia kuingia kwenye chumba cha mitihani na vifaa visivyo ruhusiwa.

 

Kufikia Jumanne, serikali ilikuwa imechukua zaidi ya vifaa 832 vya kigeni katika vituo vya mitihani ikiwa ni pamoja na simu za rununu na karatasi bandia.