Kukejeli Uhuru; mwanaharakati aachiliwa kwa dhamana

Muhtasari

• Polisi walikuwa wameomba siku 14 kuendelea kumzuilia Edwin Mutemi Kiama ili wakamilishe uchunguzi.

• Aliagiza Kiama kuweka mahakamani dhamana ya Shilingi laki tano pesa taslimu na aripoti kwa afisa wa uchunguzi kila siku kwa siku kumi.

Mwanaharakati Edwin Kiama akiwa mahakamani siku ya Jumatano
Edwin Kiama Mwanaharakati Edwin Kiama akiwa mahakamani siku ya Jumatano
Image: Carolyne Kubwa

Mwanaharakati aliyekamatwa kwa madai ya kusambaza bango la Uhuru Kenyatta ameachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu Shilingi 500,000 akisubiri uchunguzi kukamilika.

Polisi walikuwa wameomba siku 14 kuendelea kumzuilia Edwin Mutemi Kiama ili wakamilishe uchunguzi.

Lakini hakimu Mkazi mwandamizi wa Milimani Jane Kamau siku ya Alhamisi alikataa ombi la upande wa mashtaka, akisema hakuna sababu za za kutosha zilizowasilishwa mbele ya mahakama kuidhinisha kuzuiliwa kwa mshukiwa.

"Upande wa mashtaka umeshindwa kudhihirishia mahakama kwamba Kiama anapaswa kufungiwa wakati wa uchunguzi," alisema hakimu.

Aliagiza Kiama kuweka mahakamani dhamana ya Shilingi laki tano pesa taslimu na aripoti kwa afisa wa uchunguzi kila siku kwa siku kumi.

Aliamuru kesi hiyo kutajwa mnamo Aprili 17, kwa maagizo zaidi.