Muigizaji Ainea Ojiambo asubiri ripoti ya polisi kuhusu tukio la ufyatulianaji wa risasi

Muhtasari

• Muigizaji Ainea Ojiambo aliachiliwa Ijumaa usiku na polisi baada ya kuhusika katika tukio la ufyatulianaji risasi katikati mwa jiji la Nairobi.

Muigizaji Ainea Ojiambo
Muigizaji Ainea Ojiambo

Muigizaji Ainea Ojiambo aliachiliwa Ijumaa usiku na polisi baada ya kuhusika katika tukio la ufyatulianaji risasi katikati mwa jiji la Nairobi.

Ojiambo huigiza katika kipindi cha ‘Makutano Junction’ na anajulikana kama Nyoka. Yeye ni mmiliki wa bunduki mwenye leseni.

Alipewa dhamana ya polisi huku uchunguzi kuhusu kisa hicho kilichotokea katika barabara ya Moi ukiendelea.

Mlinzi na mtu mwingine aliyekuwa amesimama walipigwa risasi na kujeruhiwa vibaya katika tukio hilo la ufyatulianaji risasi.

Mlinzi huyo alipigwa risasi kwa jicho huku mhasiriwa mwingine akupatwa na risasi kiunoni, baada ya Ojiambo kufyatua risasi wakati akipambana na genge la watu watatu ambao walitaka kuiba ushanga wake.

Mlinzi huyo alifariki akiwa hospitalini, maafisa walisema. Tukio hilo lilitokea Ijumaa saa kumi unusu jioni. Ojiambo alikuwa akizungumza na mwanamke asiyejulikana wakati wavamizi walimposhambulia.

Eneo hilo kawaida huwa na watu wengi. Ojiambo aliripoti kwa polisi siku ya Jumamosi kuhusu tukio hilo.

Polisi waliandika taarifa yake pamoja na watu wengine watano walioshuhudia tukio hilo. Ripoti ya uchunguzi itapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka.

"Tutajua njia ya kusonga mbele baada ya DPP kutoa uamuzi wake kuhusu ripoti ya uchunguzi," afisa wa uchunguzi alisema.

Iliibuka mtu wa tatu anayeaminika kuwa mmoja wa watu waliomshambulia Ojiambo alipigwa risasi na kujeruhiwa. Bado hajatafuta matibabu.