Mzozo wa DRC: Waasi waua watu 19 wakiwemo wanajeshi 10 mashariki mwa DRC

Muhtasari

• Mzozo wa DRC: Umwagikaji wa damu waendelea mashariki mwa DRC muda mfupi baada ya rais kutangaza 'hali ya kuzingirwa' kwa mikoa miwili

Image: AFP

Wapiginaji wenye silaha wamewaua takriban watu 19 wakiwemo wanajeshi kumi baada ya kushambulia vijiji viwili mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo siku ya jumamosi muda muda mfupi baada ya Rais Felix Tshisekedi kutangaza kwamba mikoa miwili mashariki mwa nchi hiyo Ituri na Kivu Kaskazini ,imezingirwa .

Ongezeko la mashambulizi ya makundi yaliyojihami na machafuko ya kikabila yamesababisha vifo vya watu Zaidi ya 300 tangu mwanzoni mwa mwaka huu huku wanajeshi wa serikali na walinda amani wa umoja wa mataifa wakijaribu kuleta utulivu mashariki mwa nchi hiyo .

Shambulio la hivi punde limefanyika siku ya jumamosi wakati wapiganaji wenye silaha waliposhambulia vijiji viwili katika mji wa Kivu kaskazini wa Beni, mamlaka za jimbo hilo zimesema

Baadaye siku hiyo imam mwenye ushawishi mkubwa aliuawa kwa kupigwa risasi msikitini mjini Beni alipokuwa akiwaswalisha watu wakati wa jioni . Alitambulika kwa kupinga itikadi kali za kidini kupitia kitu kimoja cha redio katika jimbo hilo.

Image: GOOGLE

" Lengo ni kumaliza kabisa ghasia ambazo zimesababisha mauaji ya wananchi katika sehemu hii ya taifa kila siku' amesema msemaji wa serikali Patrick Muyaya ambaye hakubainisha kitakachofuata baada ya hali hiyo kutangazwa katika mikoa hiyo miwili .

Siku ya ijumaa Polisi katika mji wa Beni waliwatawanya wanafunzi waliokuwa wakifanya maandamano ya kuketi katika ukumbi mmoja wa mji humo kulalamikia ongezeko la hali ya ukosefu wa usalama.

Watu kadhaa walijeruhiwa na wengine kukamatwa kulingana na shahidi mmoja aliyezungumza na shirika la habari la Reuters.

Ni makundi yapi yanayotekeleza mauaji?

Kundi moja la waasi kutoka Uganda kwa jina Allied Democratic Forces (ADF) limekuwa mashariki mwa DRC tangu miaka ya 1990 na linaaminika kuhusika na visa vingi vya mashambulizi katika eneo hilo .

Kundi hilo limefanya msururu wa mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya raia tangu jeshi lilipoanza oparesheni ya kuliangamiza mwaka wa 2019 na liliwaua watu 850 mwaka jana kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa .

Ghasia hizo zimesababisha mgogoro wa kibinadamu mashariki mwa DRC ambapo Zaidi ya watu milioni 1.6 wameachwa bila makazi huko Ituri ,mkoa wenye jumla ya watu milioni 5.7 shirika la UNICEF lilisema mwezi Aprili . Watu wengine miloni 2.8 wanahitaji usaidizi wa dharura ,shirika hilo lilisema .

Mauaji ya Sheikh Ali Amini

Tovuti moja, Politico.cd imedai kwamba Imam Sheikh Al Amini aliuawa na wapiganaji wa kundi la ADF kwa sababu ya kulipinga kundi hilo .

Sheikh Ali Amini alikuwa akisikika redioni kila mara akipinga ghasia za wanachama wa ADF ambalo limeendelea kutekeleza mashambullio katika ngome yake ya Beni.

Alikuwa amehojiwa na mamlaka tarehe 4 Aprili kuhusu vitisho alivyokuwa akivipata kutoka kwa kundi hilo .

Image: GETTY IMAGES

Kudi la Islamic State limedai kuhusika na Mashambulizi mengi ya ADF ambalo lilianza kuonekana mashariki mwa DRC Aprili mwaka wa 2019 . Operesheni inayoendelea ya kijeshi imeshindwa kuyamaliza kabisa makundi ya wapiganaji wanaohudumu katika maeneo hayo kwa miongo kadhaa sasa .