SIASA ZA BBI

Lazima tubadilishe katiba mpende msipende! Babu awaambia majaji

Mbunge wa Embakasi akashifu majaji kwa kupuuzilia mbali mchakato wa BBI

Muhtasari

•Babu Owino asema kuwa muswada wa BBI unajali maslahi ya Wakenya.

•Adai kuwa hawatarudi nyuma kwenye nia yao ya kubadilisha katiba.

Mbunge wa Embakasi ya Mashariki, Babu Owino
Mbunge wa Embakasi ya Mashariki, Babu Owino

Mbunge wa Embakasi ya mashariki Babu Owino ametangaza kuwa ni lazima  katiba itabadilishwa.

Kupitia kurasa zake kwenye mitandao ya kijamii ya Facebook na Twitter, mbunge huyo anayekumbwa na sarakasi si haba siasani amesema hawatorudi nyuma kwenye nia yao ya kubadilisha katiba kupitia mswada wa BBI.

Babu ametangaza matamshi haya siku moja baada ya mahakama kuu ya Kenya kutupilia mbali mchakato mzima wa BBI.

“Tutabadilisha katiba majaji wapende wasipende. Muswada huo unajali maslahi ya Wakenya.” Babu aliandika kwenye akaunti yake ya Twitter siku ya Ijumaa.

Siku ya Alhamisi, mahakama ilikosoa hatua ya Rais Kenyatta kuongoza mchakato wa BBI huku majaji wakidai kuwa shughuli hiyo ilifaa kumilikiwa na wananchi na wala sio rais mwenyewe.

Majaji hao pia walikosoa hoja ya kuongeza maeneo bunge sabini huku wakiashiria kuwa kisheria hiyo ni kazi ya tume la IEBC wala sio jopo liliteuliwa na Rais.

Babu Owino ambaye ni mwandani mkubwa wa kinara wa ODM, Raila Odinga amekuwa kwenye mstari wa mbele katika kupigia debe mchakato wa BBI.

Mbunge huyo wa mara ya kwanza na aliyekuwa kiongozi wa muungano wa wanafunzi wa chuo kikuu cha Nairobi(UON) kwa muda mrefu anajulikana kuwa na ujasiri mwingi anapoongea.