SIASA ZA MLIMA KENYA

Viongozi wa Mlima Kenya waanza juhudi za kuunganisha eneo

Kikundi cha viongozi kutoka eneo la mlima Kenya kilikutana kuzungumza maslahi ya eneo hilo na kuapa kuleta pamoja eneo nzima nchi inapokaribia uchaguzi

Muhtasari

•Kabogo alisema kuwa katiba imeruhusu eneo hilo kuteua mgombeaji wa kiti cha urais.

•Mkutano mwingine utakaohusisha viongozi zaidi umepangwa kufanyika Nyeri baada ya wiki mbili

Viongozi wa Mlima Kenya
Viongozi wa Mlima Kenya
Image: EZEKIEL AMING'A

Kikundi cha viongozi kutoka eneo la mlima kimeapa kuanza juhudi za kuunganisha eneo hilo tunapokaribia uchaguzi mwaka ujao.

Kikundi hicho ambacho kilikutana jijini Nairobi siku ya Jumatano ili kujadili maslahi ya eneo hilo ambalo lina wapiga kura wengi zaidi  kilitangaza kuwa mikutano ya kuunganisha eneo hilo itaanza huku mkutano wa kwanza ukipangiwa kufanyika Nyeri baada ya wiki mbili.

Viongozi wa ngazi tofauti ikiwemo Gavana Mwangi wa Iria wa Muranga, Mutahi Kahiga wa Nyeri, Anne Mumbi wa Kirinyaga, Lee Kinyajui wa Nakuru, aliyekuwa gavana wa Kiambu William Kabogo, aliyekuwa mbunge wa Dagorreti Kusini Dennis Waweru kati ya wengine waliongelesha wanahabari baada ya mkutano wao.

Wakiongozwa na gavana wa Murang’a Mwangi wa Iria, viongozi hao walisema kuwa walikubaliana kupatana kwa ghafla na kuwa huo ndio mwanzo tu wa mikutano wingi wanayotaka kufanya na kushirikisha viongozi wengi ili kujadili watakavyounganisha eneo hilo.

“Tulikuja pamoja kwani tuko katika eneo moja na tuko imara.Tunataka kuhakikisha kuwa eneo la Mlima Kenya limeungana pamoja na kuendeleza  lengo moja. Kura yenye ni ya maana na haitagawanywa na yeyote” Alisema Mwangi.

Aliyekuwa gavana wa kaunti ya Kiambu, William Kabogo alijivunia wingi wa wapiga kura walio katika eneo hilo huku akidai kuwa kura zao zina maana sana kwenye siasa za Kenya.

Nguvu yetu kama eneo la mlima Kenya ni wingi wa watu ambao wako pamoja. Tumeanza safari ya kujipanga tutakavyosonga mbele na huu ni mwanzo tu, tutahusisha viongozi wengine wengi” Kabogo alisema.

GAVANA MWANGI WA IRIA
GAVANA MWANGI WA IRIA
Image: FILE

Kabogo alisema kuwa katiba imeruhusu eneo hilo kuteua mgombeaji wa kiti cha urais.

“Tutazungumza sisi kama viongozi wa Mlima Kenya na tukiona ni vyema kusukuma mmoja wetu, bila shaka msishangae mkiskia kuna mmoja wetu amesimama” Kabogo alisema

Viongozi hao walitangaza kuwa watafanya mkutano mwingine utakaohusisha viongozi wengi zaidi kutoka eneo hilo baada ya wiki mbili. Mkutano huo unatarajiwa kufanyika Nyeri huku gavana wa eneo hilo, Mutahi Kahiga akialika viongozi zaidi kujitokeza kwenye mkutano huo.

“Tumepanga mkutano mwingine kufanyika baada ya wiki mbili. Mkutano huo utahusisha watu zaidi na tutaanza shughuliya kuwafikia. Hivi karibuni tutazungumza lugha moja. Kikwetu tunasema, watu ambao hawakopamoja hupigwa na fimbo moja. Tunataka kuwa pamoja kwani wingi wetu  ni wa umuhimu" Gavana Waiguru alisisitiza.