Video inayoonyesha polisi akipokonywa simu Roysambu ni bandia -NPS

Upelelezi wa polisi umebaini kuwa tukio hilo halikutendeka na video hiyo ilikuwa imetengenezwa kwa kompyuta.

Muhtasari

•Video ambayo ilisambazwa sana mitandaoni siku ya Jumatano ilionyesha alionekana kuwa  afisa wa polisi akizungumza kwa simu akiwa amesimama kwenye barabara iliyo katika mzunguko wa Roysambu.

•Kulingana na ujumbe uliochapishwa kwenye akaunti rasmi ya NPS katika mtandao wa Twitter mida ya  saa nne kasorobo usiku wa Jumatano, upelelezi ulibaini kuwa tukio hilo halikutendeka na video hiyo ilikuwa  imetengenezwa kwa kompyuta.

Image: HISANI

Video inayoenezwa mitandaoni ikionyesha afisa  wa polisi akiibiwa simu na mtu aliyeabiri pikipiki ni ghushi, huduma ya polisi nchini Kenya(NPS) imedhihirisha.

Video ambayo ilisambazwa sana mitandaoni siku ya Jumatano ilionyesha alionekana kuwa  afisa wa polisi akizungumza kwa simu akiwa amesimama kwenye barabara iliyo katika mzunguko wa Roysambu.

Afisa huyo anapoendelea kupiga simu, pikipiki iliyokuwa imebeba abiria wawili ilionekana kupita mbele yake na abiria aliyekuwa amekaa nyuma alionekana kunyakua simu ambayo afisa huyo alikuwa ameshika kwenye masikio.

Video hiyo ilisisimua wanamitandao wengi ambao waliisambaza kabisa kweli na kuibua gumzo kote nchini. 

Hata hivyo, NPS inayoongozwa na Inspekta Jenerali Hilary Mutyambai wamejitokeza kupinga uhalali wa tukio hilo.

Kulingana na ujumbe uliochapishwa kwenye akaunti rasmi ya NPS katika mtandao wa Twitter mida ya  saa nne kasorobo usiku wa Jumatano, upelelezi ulibaini kuwa tukio hilo halikutendeka na video hiyo ilikuwa  imetengenezwa kwa kompyuta.

"Upelelezi wetu umeonyesha kuwa video ambayo inaenea mitandaoni ikionyesha afisa wa polisi akipokonywa simu ni ghushi na ina malengo mabaya. Tunasihi umma kuipuuzilia  mbali" NPS waliandika.

Wakenya wengi ambao hawakuonekana kushawishika na ujumbe huo walimwaga hisia zao chini ya ujumbe huo huku wengi wakisisitiza kuwa tukio hilo ni la kweli.