SIASA ZA 2022

'Nilijihusisha na UDA kwa kukosa hali Jubilee' Ruto ataja sababu zake kutojihusisha tena na Jubilee

Ruto hata hivyo alimpongeza Raila kwa kuweza kujumuisha jamii mbalimbali katika chama chake cha ODM.

Muhtasari

•Akizungumza na Gidi katika kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi siku ya Jumanne, Ruto amesema kuwa watu ambao rais Uhuru Kenyatta alipatia fursa ya kuendeleza chama wamekisambaratisha.

•Alisema kuwa salamu kati ya rais Kenyatta na kinara wa ODM zilichangia pakubwa katika kusambaratisha chama.

Naibu rais William Ruto akizungumza na Gidi siku ya Jumanne
Naibu rais William Ruto akizungumza na Gidi siku ya Jumanne
Image: RADIO JAMBO

Naibu rais William Ruto ametaja kukosa hali katika chama cha Jubilee kama sababu yake kubwa kujihusisha na chama cha UDA.

Ruto ambaye ameashiria nia yake ya kuwania kiti cha urais mwaka ujao  amesema kuwa fujo ambayo ilijitokeza ndani ya  chama tawala cha Jubilee ilimsukuma nje.

Akizungumza na Gidi katika kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi siku ya Jumanne, Ruto amesema kuwa watu ambao rais Uhuru Kenyatta alipatia fursa ya kuendeleza chama wamekisambaratisha.

"Pale Jubilee kumetokea kizungumkuti kikubwa cha  fujo. Wale watu ambao rais aliwaachia nafasi ya kuendesha chama wamekisambaratisha" Ruto alisema.

Ruto ametaja kugura kwa wanachama kama baadhi ya masaibu ambayo yameshuhudiwa katika chama cha Jubilee. Amesema kuwa chama hicho kimepoteza zaidi ya wabunge mia moja tangu mwanzo wa utawala wake.

"Chama ambacho kilikuwa na zaidi ya wabunge mia mbili sasa huwezi kuhesabu wabunge thelathini" Naibu rais alisema.

Naibu rais alieleza kuwa hapo awali alikuwa amejihusisha na uundaji wa Jubilee kwani alitaka kusaidia katika kuangamiza ukabila ila hali ikabadilika baada ya 'handshake'. 

Alisema kuwa salamu kati ya rais Kenyatta na kinara wa ODM zilichangia pakubwa katika kusambaratisha chama.

'Tulipoteza nafasi kubwa sana pale Jubilee wakati wale waliteka nyara Jubilee wakawa ni watu ambao hawaelewi chochote. Ni kama sasa kazi yao kubwa ni kufurusha watu"  Alisema.

Naibu rais alisema kuwa UDA iliundwa kwa sababu wanachama wengi wa Jubilee hawakuwa tayari kujiunga na ODM kama ilivyoonekana.

Ruto alisema kuwa nia ya UDA ni kuunganisha Wakenya kutoka jamii mbalimbali nchini. 

"Pale katika UDA sasa utakuta wabunge wa Pwani, Kaskazini mashariki, eneo la kati, Bonde la Ufa, Nyanza, Magharibi.. kwa hivyo tumetangamana pale. Hivyo ndivyo siasa inafaa kuendeshwa." alisema Ruto.

Alisema kuwa ana matarajio kuwa wengi katika chama cha Jubilee watajiunga na UDA kuanzia mwezi wa Desemba.

Ruto hata hivyo alisifia chama cha ODM kinachoongozwa na mpinzani wake mkubwa Raila Odinga na kukitaja kama chama ambacho hakina ukabila.

Alimpongeza Raila kwa kuweza kujumuisha jamii mbalimbali katika chama chake cha ODM.

"Ni lazima nimpongeze aliyekuwa waziri mkuu kwa kujaribu kuunda chama na kushikilia chama kiwe chama cha kitaifa. Angalau katika chama cha ODM kuna mbunge kutoka eneo la Magharibi. Kuna mbunge kutoka Pwani... inaonekana kina sura ambayo si mbaya sana ila hakifikii kile chama tulichokuwa nacho cha Jubilee tulikuwa na wabunge katika kaunti 41" Ruto alisema.

Ruto alivikosoa vyama vya kijamii na kusema kuwa ndivyo vinaharibu siasa za Kenya.

"Siasa zinafaa kuendeshwa sio kwa misingi ya kikabila, ni kuunganisha watu" naibu rais alisema.

Ruto hata hivyo alisita kuzungumzia swala la atakayekuwa mgombea mwenza wake na kusema kuwa watajadiliana hayo na viongozi wa UDA pamoja na wanachama.