KESI YA TECRA MUIGAI

Walipendana sana! Nduguye Omar Lali atoa ushahidi kuhusiana na kifo cha mrithi wa Keroche

Quswai alisema kuwa alimpata Tecra akiwa amelala chini huku ameangalia juu.

Muhtasari

• Quswai Lali ambaye ni mfanyakazi katika mkahawa wa Peponi alisema kuwa nduguye alimpigia simu mida ya saa kumi na mbili kasorobo asubuhi na kumuarifu afike kwake.

•Alieleza kuwa Tecra alikuwa akivunja damu kutoka kwenye sikio lake la kushoto na kulikuwa na matone ya damu karibu na yeye.

Tecra na Lali
Tecra na Lali
Image: Maktaba

Nduguye Omar Lali aliyekuwa mpenzi wa mridhi wa Keroche Bi Tecra Muigai  na ambaye ni mshukiwa kwenye mauaji yake ameeleza mahakama kuwa wawili hao walipendana sana na hakuwahi ona wakipigana.

Akitoa ushahidi wake mahakamani siku ya Jumatano, Quswai Lali ambaye ni mfanyakazi katika mkahawa wa Peponi alisema kuwa nduguye alimpigia simu mida ya saa kumi na mbili kasorobo asubuhi na kumuarifu afike kwake.

Jambo hilo lilimshangaza sana kwani haikuwa kawaida ya Omar kumpigia masaa kama yale. Wawili hao wanaishi umbali  wa hatua chache kutoka kwa mwingine.

"Nilishangaa sana, haikuwa kawaida yake kunipigia simu masaa hayo. Nikaenda pale na akanifungulia mlango" Quswai alieleza mahakama

Quswai alisema kuwa alimpata Tecra akiwa amelala chini huku ameangalia juu.  Kwa wakati huo, nduguye alionekana kachanganyikiwa na mwenye wasiwasi.

"Tukampatia Tecra huduma ya kwanza na akaanza kupiga nduru ila haingesikika vizuri. Nikampigia daktari May Makau ila akasema kuwa alikuwa anawajibikia  jukumu lingine" Quaswai aliendelea kusema.

Alieleza kuwa Tecra alikuwa akivunja damu kutoka kwenye sikio lake la kushoto na kulikuwa na matone ya damu karibu na yeye.

Hapo akapigia shemeji yake Ali Bakari akaja na watu wawili na wakashirikiana kumpeleka Tecra kwenye zahanati iliyokuwa karibu.

"Aliporejesha fahamu, tulimpeleka King Fahad kwa boti na akapewa dawa za kupunguza pombe mwilini. Tulikaa pale hospitali hadi saa kumi na moja jioni wakati ambapo mwanamke kwa jina Monica Maharubu alikuja. Alikuwa ametumwa na mamaye Tecra, Tabitha Karanja." Quaswai alisema.

Kulingana na Quaswai, Maharubu kwa ushirikiano na madaktari ndio walipanga namna ya kumpeleka Tecra Nairobi kwa matibabu zaidi.

Quaswai alisema kuwa hakushuhudia ajali iliyotokea, Lali ndiye aliyemweleza yaliyojiri.

Alisema kuwa hawakupiga ripoti kwani walidhani ni ajali ndogo tu ilikuwa imetokea na angepata nafuu.