Vurugu Kiambaa baada ya Jubilee kudai kuwepo kwa ulaghai katika uhesabu wa kura

Muhtasari

•Kufikia sasa Njuguna wa UDA anaongoza akiwa na kura 21,606 huku akifuatwa kwa karibu na Kariri Njama wa Jubilee akiwa na kura 21, 151.

Image: HISANI

Huku ikiwa imebaki kutangazwa kwa matokeo ya kituo cha kupigia kura kimoja tu ili mshindi wa kinyang'anyiro cha Kiambaa ajulikane, vurugu zimeshuhudiwa katika kituo cha kuhesabia kura cha Karuri baada ya mgombea kiti na tikiti ya Jubilee kudai kuwepo kwa wizi wa kura.

Kariri Njama akiungwa mkono na wafuasi wake wamekabiliana na maafisa wa usalama wakiagiza kuhesabiwa tena kwa kura za vituo vitatu.

Mwanasiasa huyo na wafuasi wake hawakuridhishwa na matokeo ambayo yalitangazwa kutoka vituo vya Cianda, Gachie na Muchatha. Walidai kuwa matokeo yalikuwa yamebadilishwa kwa mapendeleo mgombea kiti na tikiti ya UDA John Njuguna.

Kufikia sasa Njuguna wa UDA anaongoza akiwa na kura 21,606 huku akifuatwa kwa karibu na Kariri Njama wa Jubilee akiwa na kura 21, 151.

Matokeo rasmi yanatarajiwa kutangazwa baada ya kujumuishwa kwa matokeo ya kituo cha mwisho kilichobaki.