Jamaa atapeli mseja pensheni ya 780,050 kwa kumbubujikia maneno matamu na kuahidi kumuoa

Bila kufahamu chochote kuhusu njama ya tapeli huyo, mwanamke yule ambaye alikuwa amechizishwa na mapenzi matamu ya jamaa huyo alimkabidhi pensheni yake yote.

Muhtasari

•Wycliffe Amakobe Omunga anadaiwa kuwa na mazoea ya kulenga wanawake walio pweke wanaokaribia kupokea pensheni zao na kuwabubujikia maneno matamu ya mapenzi huku akiwaahidi ndoa kunjufu baada ya kustaafu kwao.

Image: TWITTER//DCI

Polisi wanamzuilia mwanaume mmoja anayedaiwa kuwa na mazoea ya kulenga wanawake walio pweke wanaokaribia kupokea pensheni zao na kuwabubujikia maneno matamu ya mapenzi huku akiwaahidi ndoa kunjufu baada ya kustaafu kwao.

Kwenye tukio moja, Wycliffe Amakobe Omunga anaripotwa kumshawishi mwanamke mmoja  kumpatia pensheni yake ya shilingi 780,050 ili kuanzisha biashara ya kuuza maji pamoja huku akimuahidi kwa maneno matamu kuwa wangefurahia maisha pamoja baada ya kustaafu kwake.

Bila kufahamu chochote kuhusu njama ya tapeli huyo, mwanamke yule ambaye alikuwa amechizishwa na mapenzi matamu ya jamaa huyo alimkabidhi pensheni yake yote.

Hapo ndipo mapenzi kati yao yakaanza kudidimia na jamaa akatoweka na pesa zile zote na kuzima simu mwanamke yule asiweze kumfikia tena.

Baadae aliweza kumfuatilia na kukabiliana naye akidai pesa zake ila jamaa akamwambia kuwa biashara ilikuwa imechukuliwa na kampuni ya bima kwa kukosa kulipa kiwango fulani cha pesa.

Alikamatwa siku ya Jumamosi.