Gavana Charity Ngilu aruhusiwa kwenda nyumbani baada ya kupokea matibabu ya covid-19

Muhtasari
  • Gavana Charity Ngilu aruhusiwa kuenda nyumbani baada ya kupokea matibabu ya covid-19
ngilu
ngilu

Gavana wa kaunti ya Kitui Charity Ngilu Jumatano aliruhusiwa kutoka Hospitali ya Nairobi baada ya kupokea matibabu ya Covid-19.

Kupitia kwenye ukurasa wake wa twitter aliandika;

, "Ninaondoka hospitalini baada ya kuruhusiwa, namshukuru Mungu kwa kurudisha afya yangu. Ninawashukuru pia madaktari na wafanyikazi wengine wa Kitui na Nairobi kwa huduma bora."

"Asante nyote kwa ujumbe za upendo na matakwa ya kupona haraka."Aliandika Ngilu.

Habari za ugonjwa wake zilitangazwa na gavana wa kaunti ya Machakos Alfred Mutua wakati wa tamasha la muziki siku ya jumanne.

Mkuu wa mawasiliano wa Kaunti Denis Omwange alisema Ngilu ameshauriwa kupumzika, lakini kwa jumla yuko katika hali nzuri.

“Alikuwa hajawekewa oksijeni au mashine nyingine yoyote tangu alipolazwa katika Hospitali ya Nairobi. Kwa kuwa hali yake imeimarika, ameombwa aende kupumzika nyumbani, ”Omwange alisema.

Mapema Jumatano Omwange alikuwa amesema Ngilu alikuwa akiitikia vyema matibabu na "hakuwa katika hatari yoyote inayoonekana."