Kuungana na Ruto la hasha! Raila asema

Muhtasari

• Odinga amesema kuna uwezekano finye mno yeye kufanya kazi na naibu rais William Ruto.

Ruto (kushoto) na Odinga (kulia), walikuwa 'maswahiba' wanaotarajia kusigana katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2022
Ruto (kushoto) na Odinga (kulia), walikuwa 'maswahiba' wanaotarajia kusigana katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2022
Image: GOOGLE

Kinara wa upinzani Raila Odinga amesema kuna uwezekano finye mno yeye kufanya kazi na naibu rais William Ruto.

Akizungumza katika mahojiano na vituo vya radio vya lugha ya Kikuyu siku ya Ijumaa Raila alisema anaweza tu kufanya kazi na mtu ambaye sera zao zinaambatana.

Raila alieleza nyakati ambazo amefanya kazi na naibu rais na changamoto ambazo ziliibuka akisema kwamba walikuwa pamoja katika chama cha ODM na hata akamteua kuwa waziri wa kilimo lakini akamhamisha hadi wizara ya elimu ya juu kutokana na sakata katika wizara hiyo.

Kinara huyo wa ODM pia alisema hulka ya naibu rais kutokuwa na msimamo na kupinga mambo hata yale ambayo yeye mwenyewe alihusika katika uamuzi wake yanafanya iwe vigumu wao kufanya kazi pamoja.  Alitaja wakati wa marekebisho ya katiba akisema Ruto alikuwa mmoja wa wanachama wa kamati iliyobadilisha mapendekezo ya Bomas walipokutana Naivasha na kisha akageuka na kupinga tena mapendekezo yake wakati wa kura ya maamuzi ya katiba ya 2010.

KInara wa ODM Raila Odinga
Image: Maktaba

Kuhusu uungwaji mkono na watu wa Mlima Kenya, Raila alipuuzilia mbali madai kwamba hawezi kuungwa mkono na watu wa eneo hilo akisema kwamba amefanya kazi kwa miaka mingi na watu kutoka jamii ya Agikuyu.

Alisema familia yake kuanzia kwa babake Jaramogi Oginga Odinga aliyeongoza shinikizo za kutaka hayati mzee Jomo Kenyatta aachiliwe kutoka korokoroni. Kiongozi huyo wa upinzani pia alisema wanawe wawili wa kiume marehemu Fidel na Raila Junior walioa kutoka Mlima Kenya.

Kuhusu hali ya kiuchumi ya taifa kinara wa ODM alitaja ubadhirifu wa pesa katika serikali kama chanzo cha matatizo ya kiuchumi yanayokumba nchi.

Alisema taifa lilikuwa limekopa pesa nyingi ambazo badala ya kutumika kwa miradi ya kuimarisha uchumi zimekuwa zikiishia mifukoni mwa maafisa wachache wafisadi.

Pia alikosoa sera ya kifedha iliyotumika katika kuchukuwa mikopo akisema kwamba ilipelekea serikali kuchukuwa mikopo ambayo riba zake ni ghali muno na muda wa kulipa ni mfupi hali ambayo imefanya mikopo ya serikali kuwa ghali mno kwa uchumi wa taifa.

Katika ubadhirifu wa pesa za umma Raila alitaja kandarasi ya ujenzi wa reli ya kisasa SGR akisema kwamba kandarasi hiyo iliyongezwa kwa zaidi ya dola bilioni moja ikilinganishwa na kandarasi iliyokuwa imetiwa saini na serikali yake na rais Mustaafu Mwai Kibaki.