Aliyekuwa mbunge wa Likoni Salim Mwavumo aaga dunia

Mwavumo ambaye alikuwa anahudumu kama kiongozi wa baraza la wazee la Likoni Wamiji alifariki akiwa nyumbani kwake maeneo ya Kizingo alfajiri ya Jumatatu

Muhtasari

•Mwanasiasa Suleiman Shahbal alithibitisha msiba huo kupitia ukurasa wake wa Facebookna kusema kuwa kifo cha mzee Mwavumo kilivunja moyo wake kwani alikuwa kama baba kwake.

Image: FACEBOOK// SULEIMAN SHAHBAL

Aliyekuwa mbunge wa eneo bunge la Likoni kati ya mwaka wa 1992-1997 Salim Khalif Mwavumo ameaga dunia.

Mwavumo ambaye alikuwa anahudumu kama kiongozi wa baraza la wazee la Likoni Wamiji alifariki akiwa nyumbani kwake maeneo ya Kizingo alfajiri ya Jumatatu. 

Mwanasiasa Suleiman Shahbal alithibitisha msiba huo kupitia ukurasa wake wa Facebookna kusema kuwa kifo cha mzee Mwavumo kilivunja moyo wake kwani alikuwa kama baba kwake.

"Nimepokea habari za kifo cha Mzee Salim Mwavumo, kiongozi wa baraza la wazee la Likoni Wamji na huzuni nyingi. Mzee Mwavumo ambaye pia alihudumu kama mbunge wa Likoni alikuwa kama baba kwangu. Alihudumu pamoja na baba yangu kama mjumbe katika manispa ya Mombasa miaka ya 1960's. Namheshimu na nathamini mawaidha yake ya busara.

Likoni na Mombasa kwa jumla imeondokewa na mzee aliyekuwa mwingi wa hekima. Mungu aiweke roho yake mahali pema penye wema." Shahbal aliandika.

Bado haijabainika kilichosababisha kifo cha Mwavumo. Mungu aulaze moyo wake pema.