Simanzi Siaya baada ya polisi kuteketea ndani ya nyumba

Marehemu alikuwa peke yake ndani ya nyumba wakati moto ulitokea.

Muhtasari

•Akithibitisha tukio hilo, kamanda wa polisi katika kaunti ya Siaya Mohammed Barre amesema kuwa bado haijabainika wazi kilichosababisha mkasa ule.

•Inaripotiwa kuwa polisi wenzake waliweza kuokoa mali yao kabla ya moto ule kuenea na kufikia nyumba zao.

Eneo la tukio
Eneo la tukio
Image: DICKENS WASONGA

Habari na Dickens Wasonga

Sajini mwandamizi wa polisi katika kituo kimoja cha polisi kaunti ya Siaya amepoteza maisha yake baada ya nyumba aliyokuwa ndani kuteketea mida ya saa tatu kasorobo asubuhi ya Alhamisi.

Akithibitisha tukio hilo, kamanda wa polisi katika kaunti ya Siaya Mohammed Barre amesema kuwa bado haijabainika wazi kilichosababisha mkasa ule.

Barre ameeleza kuwa wazimato kutoka kaunti ya Siaya waliitwa kuzima moto ule ila afisa aliyekuwa ndani alikuwa ameaga tayari.

"Hatujui kilichotokea ila tunachokijua ni kwamba afisa wetu alikufia pale ndani" Barre alisema.

Mkuu huyo wa polisi amesema kuwa uchunguzi unaendelea ili kubaini wazi kilichotokea pale.

Kulingana na kamanda wa polisi maeneo ya Siaya ya kati Bw Benedict Mwangangi, marehemu alikuwa peke yake ndani ya nyumba wakati moto ulitokea.

Inaripotiwa kuwa polisi wenzake waliweza kuokoa mali yao kabla ya moto ule kuenea na kufikia nyumba zao.

Jina la afisa aliyeangamia litafichuliwa baada ya familia yake kufahamishwa. Marehemu alipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Siaya.