Kenya yapokea msaada wa dozi 880,320 zaidi za chanjo ya Moderna kutoka Marekani

Chanjo hizo ziliwasili katika uwanja wa ndege wa JKIA asubuhi ya Jumatatu

Muhtasari

•Hii ni shehena ya pili ya dozi hizo kuwasili nchini kama sehemu ya msaada wa dozi milioni 1.76 kutoka Marekani. 

•Wiki mbili zilizopita shehena ya kwanza ya dozi 880,460 za chanjo ya Moderna ziliwasili nchini kutoka Marekani.

Image: TWITTER// MoH

Kenya imepokea dozi 880,320 zaidi za chanjo dhidi ya virusi vya Corona aina ya Moderna .

Hii ni shehena ya pili ya dozi hizo kuwasili nchini kama sehemu ya msaada wa dozi milioni 1.76 kutoka Marekani. 

Chanjo hizo ziliwasili katika uwanja wa ndege wa JKIA asubuhi ya Jumatatu na kupokewa na Mshirikishi wa wizara ya afya Rashid Aman.

Taarifa hiyo ilitolewa  na wizara ya Afya nchini kupitia mtandao wa Twitter.

"Msaada wa dozi 880,000 za Moderna umeswasili nchini kutoka Marekani asubuhi ya leo. CAS wa Afya Dkt Rashid Aman amezipokea kwa niaba ya waziri Mutahi Kagwe"  Wizara ya Afya ilitangaza.

Alipokuwa anapokea dozi hizo Dkt Aman amehimiza watu ambao hawajapokea chanjo kujitokeza ili kupata kuona kuwa sasa kuna dozi zaidi. Wale ambao wamepokea dozi moja pia wamehimizwa kujitokeza kupokea ya pili.

"Ili tuweze kufungua uchumi wetu inafaa tuweze kuwa na kinga miongoni mwa makundi ama tuwe tumechanja watu wote" Aman alisema.

Wiki mbili zilizopita shehena ya kwanza ya dozi 880,460 za chanjo ya Moderna ziliwasili nchini kutoka Marekani.

Mnamo Ijumaa wiki iliyopita Kenya ilipokea shehena ya kwanza ya dozi 141,000 za chanjo aina ya Johnson & Johnson.

Kufikia sasa Kenya imepokea dozi 5, 146,780 za chanjo dhidi ya Corona.